Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madagascar: Hatua za kuwezesha kukabiliana na madhara ya El Niño

Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Janga la Tabinachi Reena Ghelani (kulia) akizungumza na wakulima kwenye shamba la mtama huko kusini mwa Madagascar
© UNOCHA/Priscilla Lecomte
Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Janga la Tabinachi Reena Ghelani (kulia) akizungumza na wakulima kwenye shamba la mtama huko kusini mwa Madagascar

Madagascar: Hatua za kuwezesha kukabiliana na madhara ya El Niño

Tabianchi na mazingira

El Niño ambao ni mkondo joto, ni hali ya kawaida inayotokea kwenye baharí ikihusisha joto la hewa baharini na wataalamu wanasema unaweza kuvuruga tena kwa kiasi kikubwa mienendo ya hali ya hewa duniani. Hata hivyo dharura ya tabianchi inayosababishwa na shughuli za binadamu zinaongeza ukali na madhara ya El Niño kwa watu na sayari dunia.

Nchini Madagascar, kisiwa ambacho eneo ambamo kimo baharini linakiweka kwenye hatari ya kukumbwa na hali mbaya hewa kupindukia, Umoja wa Mataifa unashirikiana na mamlaka kusaidia taifa hilo kuhimili na kukabili.

Katika miaka ya karibuni, Madagascar imepigwa na vimbunga vikubwa kupindukia, halikadhalika  ukame mkali katika miongo minne iliyopita, na kusababisha njaa na maelfu ya wananchi kukaribia kutumbukia kwenye baa la njaa.

Kutokana na hali hiyo, Reena Ghelani, ambaye ni Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Janga la Tabianchi hususan hatua dhidi ya El Niño amezuri Madagascar, ambako anakagua miradi iliyobuniwa kuwezesha jamii kuwa na mnepo, na zisiathiriwe kwa kiasi kikubwa na hali mbaya za hewa. Daniel Dicknson wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa amezungumza na Bi. Ghelani na mazungumzo yao ndio makala yetu inayoletwa kwako na Idhaa ya UN wa Idhaa hii. Hapa Bi. Ghelani anaanza kwa kuelezea El Niño.

Reena Ghelani: “El Niño ni tukio la kawaida la hali ya hewa ambalo huathiri kiwango cha joto la hewa baharini. Na kutokana na janga la tabianchi, tunaweza kushuhudia ikitokea mara kwa mara na kwa kiwango kikubwa. Madhara yake yanakuwa mabaya zaidi, na kusababisha penginepo mafuriko makubwa au ukame mkali, ambao kwa sasa tunashuhudia maeneo mengi ya kusini mwa Afrika. Na kwa sababu jamii hazina muda wa kujikwamua kutoka madhara yaliyotangulia la El Nino, basi zinakuwa hatarini zaidi, na inachukua muda mrefu kwao kujikwamua.”

Idhaa ya UN: Sasa El Nino  imeathiri vipi wananchi wa Madagascar?

Reena Ghelani:  “Hawawezi kulima mazao ya chakula wanayohitaji ili waweze kuishi. Kuna madhara makubwa sana: iwapo huwezi kujilissha, basi unatuma watoto wako waende kusaka mbinu nyingine za kupata mlo, hivyo hawaendi shuleni. Hatimaye jamii zinakuwa zimechanganyikiwa hapa. Wanatueleza kuwa hawajui mustakabali wao.”

Wanawake wawili wakitazama nje kutokea kwenye kibanda cha kuuza bidhaa kijijini Ifotaka kusini mwa Madagascar
UN News/Daniel Dickinson
Wanawake wawili wakitazama nje kutokea kwenye kibanda cha kuuza bidhaa kijijini Ifotaka kusini mwa Madagascar

Idhaa ya UN: Tukiwa hapa maeneo ya mashamba kusini mwa Madagascar kutazama jinsi taifa hili la visiwani linajiandaa kwa tukio la El Niño, unaweza kuelezea unachoona?

Reena Ghelani:  “Kama jamii ya kimataifa, na serikali ni kuamua tusubiri hadi pale tuwapatie msaada wa kuokoa maisha, au tufanye kile ambacho wanafanya hapa; kusaka mbinu za kupunguza madhara, kutafiti mbegu zinazohimili ukame, jinsi ya kupatia jamii maji, na kusaka njia zingine za jamii kujipatia kipato. Hii ndio njia fanisi na nafuu ya kuwasaidia, kwa upande wa fedha na kuokoa maisha.”

Idhaa ya UN: Na mifumo ya kutoa maonyo mapema ina nafasi gani?

Reena Ghelani:  “Nchi nyingi zilizo kusini mwa Afrika kwa sasa zina mifumo hiyo  ya kutoa maonyo wakati wa hali mbaya ya hewa. Na hivyo, tunahitaji kujianda sasa. Na gharama ya kufanya utafiti huo ni nafuu mara saba kuliko kusubiri janga litokee. 

Mpango wa Katibu Mkuu wa UN wa Kutoa Maonyo Mapema kwa wote, unatekelezwa na serikali ya Madagascar, kwa usaidizi wa Umoja wa Mataifa. Huu ni ukanda ambao umepigwa na vimbunga 48 katika miaka 15 iliyopita, na ukame unatarajiwa kutokea. Mifumo ya kutoa maonyo mapema itatumika kusaidia jamii kujiandaa mapema.”

Idhaa ya UN: Nini umuhimu wa ushirikiano mzuri na wadau wa kitaifa katika kuchukua hatua mapema?

Reena Ghelani:  “Tunahitaij kuhakikisha kuwa serikali zina uwezo wa kuchukua hatua. Tunahitaji kufanya nao kazi pamoja, halikadhalika wahudumu wa kibinadamu na wadau wa maendeleo ili kupanua uwezo wetu. Pia tunahitaji kusikiliza wananchi kwani wao wanafahamu hali ya hewa, wanafahamu inabadilika na wanafahamu kinachofaa.”

Idhaa ya UN: Na hatimaye kwako wewe mafanikio mashinani yanakupatia taswira gani?

Reena Ghelani:  “Ni kuona watu hapa wana uwezo wa kujipatia kipato, wanajitegemea na watoto wao wanakwenda shuleni.”