Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW68: Tumejifunza mengi ya kumuinua mwanamke mkulima Tanzania- Bi. Maiseli

Matika Maiseli, Afisa Rasilimali Watu na Utawala TPHPA.
UN News
Matika Maiseli, Afisa Rasilimali Watu na Utawala TPHPA.

CSW68: Tumejifunza mengi ya kumuinua mwanamke mkulima Tanzania- Bi. Maiseli

Wanawake

Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya  hali  ya wanawake duniani, CSW68 umekunja jamvi hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataia jijini New York, Marekani na miongoni mwa washiriki ni Matika Maiseli, Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala kutoka Mamlaka ya Afya na Mimea na Viuatilifu, TPHPA iliyo chini ya Wizara ya Kilimo nchini Tanzania.

Assumpta Massoi wa Idhaa hii ya Umoja wa Mataifa amezungumza naye kufahamu ni nini anaondoka nacho kutoka mkutano huu uliolenga kusongesha  usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake na kutokomeza umaskini ambapo amesema wamejifunza mambo mengi sana.

Wanawake wapate huduma za viuatilifu kwa urahisi

Mosi; ni kuendelea kutengeneza mikakati ambayo mwanamke atahusika moja kwa moja. Mwanamke apate huduma kwa urahisi, huduma kama vile kupata viuatilifu bora vya kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao na vile vile jinsi ya kuvitumia, hii ina maana wataongeza uzalishaji na kupata mazao bora.

Pili ni suala la fedha, mwanamke aweze kupata huduma ya fedha kwa urahisi, “hii itamwongezea kufanya vizuri katika shughuli zake za kilimo ikiwemo kupata zana bora za kilimo.”

Alipoulizwa ni kwa vipi ukosefu wa usawa wa jinsia kwenye eneo wanaloshughulikia la afya ya mimea na viuatilifu huleta madhara gani, Afisa huyo kutoka TPHPA amesema “mama alikuwa anatumia muda mwingi sana shambani, lakini baada ya kuvuna mazao baba ndio anataka kumiliki kile kinachopatikana. Lakini pia mwanamke kutokana sheria zilizokuweko au mila kandamizi, mwanamke alikuwa hana uwezo wa kumiliki ardhi ipasavyo.”

Amesema wanashukuru kuwa maboresho ya sheria na kanuni za umiliki wa ardhi vimewezesha mwanamke kumiliki ardhi ya kilimo na akaendelea kuzalisha na kujipatia kipato.

Kwa vipi TPHPA inazingatia usawa wa kijinsia katika majukumu yake?

Bi. Maiseli akafafanua ni kwa jinsi gani wanazingatia usawa wa kijinsia kwenye mamlaka yao, amesema “tumekuwa tunatoa huduma kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika vijiji, nikimaanisha zile kazi au huduma zetu za kiufundi zinamfikia mwanamke wa chini kabisa vijijini na sehemu nyinginezo.”

Mathalani wanapokwenda kutoa huduma kama vile mafunzo ya viuatilifu “tunakuwa tunazingatia makundi maalum hasa wanawake, lakini pia tunahakikisha wanawake wanawezeshwa kulima kwa kutumia mbinu bora ili waweze kupata masoko nje ya nchi na ndani ya nchi,” amesema Afisa huyo wa TPHPA.