Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame ni ‘mwiba’ kwa wanawake wenye ulemavu

Sarah Kamau, Mwenyekiti wa Jukwaa la Watu wenye ulemavu la Jumuiya ya Madola akizungumza na Flora Nducha kandoni mwa mkutano wa CSW68 jijini New York Marekani.
UN News
Sarah Kamau, Mwenyekiti wa Jukwaa la Watu wenye ulemavu la Jumuiya ya Madola akizungumza na Flora Nducha kandoni mwa mkutano wa CSW68 jijini New York Marekani.

Ukame ni ‘mwiba’ kwa wanawake wenye ulemavu

Wanawake

Mabadiliko ya tabianchi yanakuwa na madhara makubwa zaidi kwa wanawake na wasichana wenye ulemavu kwani husababisha ukame na hivyo wanashindwa kupata maji ambayo ni muhimu sana kwa afya ya hedhi, amesema Sarah Kamau, Mwenyekiti wa Jukwaa la Watu wenye ulemavu la Jumuiya ya Madola.

Bi. Kamau alikuwa akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kandoni mwa mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya wanawake duniani, CSW68 ulioanza wiki hii hapa New York, Marekani na utaendelea kwa wiki mbili.

“Unajua uhaba wa maji unasababisha hali mbayá kwa wanawake wenye ulemavu hasa wakati wa hedhi. Wanashindwa kujisafi na hivyo kutangamana na watu wengine inakuwa vigumu,” amesema Bi. Kamau akiongeza kuwa wanahitaji usaidizi kupatiwa hayo maji.

Madhara ya tabianchi kwa wanawake wenye ulemavu, ni miongoni mwa hoja lukuki ambazo Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la watu wenye ulemavu la Jumuiya ya Madola anataka kuwasilisha kwenye mkutano huu.

Elimu na haki

Hoja nyingine ni elimu akisema kuwa wanawake wenye  ulemavu wameachwa nyuma sana kielimu. “Tunataka wapatiwe elimu stahili ili waweze kupata ajira na pia kufanya biashara na hatimaye wapate fedha za kujikimu.

“Kuna hoja kuhusu fursa ya kupata haki kwani watu wenye ulemavu wa akili wanaachwa nyuma na haki zao hazitiliwi maanani. Sheria zinawaona kama watu waliopungukiwa na akili hivyo hawawezi kupatiwa  haki zao,” ameeleza Bi. Kamau.

Usafiri na mawasiliano ni changamoto

Usafiri nao amesema ni changamoto hasa kwenye nchi zinazoendelea. “Usafiri ni mgumu hasa kama anatumia kitimwendo, hawezi kutumia usafiri wa umma kama matatu kwa kuwa hakuna mbinu ya kumwezesha kuingia kwenye usafiri.”

Amesema wana uwezo na nia ya kuweko kwenye mazingira tofauti lakini wanakwama, “unakutana hakuna mahali pa kujishika ili uweze kuingia na majengo mengi hayana njia za kutuwezesha kuingia.”

Akagusia pia mawasiliano hasa kwa viziwi akisema lugha ya ishara ni nzuri ili kusaidia mawasiliano.

Matarajio yake kwa CSW68

Bi. Kamau amesema wameandaa azimio ambalo wanaomba nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola walipitishe na hatimaye lipitishwe na fedha zitengwe kuweza kukamilisha kwani watafaidika kwani likitekelezwa litasongesha Malengo ya Maendeleo endelevu, SDGs na Mkataba wa Kimataifa wa watu wenye  ulemavu, CRPD.

Nini kifanyike?

Bi. Kamau anaamini kuwa jambo muhimu ni ushirikishaji wa watu wenye ulemavu wenyewe kwenye mipango yote inayowahusu.

“Wakihusishwa wanaweza kuzieleza serikali ni nini kifanyike haraka ili kufanikisha malengo yao. Wasiwasahau watu wenye ulemavu kwani wengi wameachwa nyuma muda mrefu, hivyo wakiwashirikisha katika kipindi hiki kilichobaki tunaweza kupata mafanikio,” ametamatisha Bi. Kamau.

Jumuiya ya Madola ni kundi linalohusisha nchi zilizokuwa makoloni ya Uingereza. Kundi hilo lina nchi 56 lakini ni nchi 50 ambazo ziko kwenye jukwaa la watu wenye ulemavu la jumuiya hiyo.