Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vinara wa elimu kutoka Tanzania wajizatiti kuhakikisha sauti za wasichana zinasikika CSW68

Zahra Salehe Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali linaloitwa ICCAO.
UN News/Anold Kayanda
Zahra Salehe Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali linaloitwa ICCAO.

Vinara wa elimu kutoka Tanzania wajizatiti kuhakikisha sauti za wasichana zinasikika CSW68

Wanawake

Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya wanawake duniani, CSW68 ukiwa umeingia siku yake ya 5 leo, Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imekuwa ikizungumza na washiriki kutoka mataifa mbalimbali. Leo ni baadhi ya washiriki kutoka Tanzania, vinara wa elimu wanaofadhiliwa na Mfuko wa Malala.

Zahra Salehe Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali linaloitwa ICCAO anaeleza ujumbe mkubwa waliokuja nao,

“Tumeletwa hapa kwa ajenda moja ya elimu na ujumbe mkubwa tuliokuja nao ni wa kuhakikisha sauti za wasichana na wanawake vijana zinasikika kwenye majukwaa makubwa kama haya CSW68 na sisi ajenda kubwa ambayo tunaiona kwa sasa ni ‘reentry’ ambayo ni ruhusa ya msichana kurudi shule baada kupitia changamoto kubwa. Tusimuache mtu nyuma kwa sababu ya sababu mbalimbali ambazo zote zimeletwa na kutokuwa na usawa wa kijinsia. Wanaendelea na wanaendelea kutimiza ndoto zao.”

Paulina Ngurumwa kutoka taasisi ya KINNAPA inayoshughulikia masuala ya elimu kwa jamii nchini Tanzania.
UN News/Anold Kayanda
Paulina Ngurumwa kutoka taasisi ya KINNAPA inayoshughulikia masuala ya elimu kwa jamii nchini Tanzania.

Paulina Ngurumwa kutoka taasisi ya KINNAPA anakubaliana na anachosema kinara wa elimu mwenzake na anasema wanapambana na vikwazo dhidi ya elimu ya wanawake ingawa bado kuna ugumu

“Hatuna mabweni, hatuna mahali pa kuwaweka kwa hiyo tunajikuta kuna mzigo mwingi. Kwa hiyo wito wetu wadau kwa ngazi ya ulimwengu, kwa ngazi ya mataifa, kwa ngazi ya taifa letu la Tanzania tushikamane tuone ni namna gani tunaweza kutafuta hata namna gani tuwapatie hawa watoto mabweni ambayo wanaweza wakasomea na wakakaa pale wakawa katika mazingira salama ili waeze kutimiza ndoto zao.”

Kutokana na changamoto kama hizo Nasra Kibukila kutoka shirika la TEN/MeT anapigia chepuo Bajeti ya nchi inayozingatia jinsia

Nasra Kibukila kutoka shirika la TEN/MeT nchini Tanzania.
UN News/Anold Kayanda
Nasra Kibukila kutoka shirika la TEN/MeT nchini Tanzania.

“Kwa sasa hivi Tanzania tumeshaanza mchakato wa kutengeneza bajeti ya mwaka 2024-2025 na kwas asa hivi iko kwenye ngazi ya wabunge. Tutakapotoka hapa, tutakayojifunza hapa tukirudi nyumbani tunaenda kuwa na mkutano pamoja na wabunge kuweza kuwaelezea yapi tumejifunza kwa jinsi gani kuwa na majeti yenye mrengo wa kijinsia na wao waweze kutusaidia kuhakikisha kuwa pale tutapakuwa na bajeti ya 2024-25inakuwa iko kwenye mrengo wa kijinsia kuweza kuhakikisha kuwa makundi yote maalumu yanakuwa yana bajeti yao kuwawezesha.”