Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na harakati za usimamizi wa matumizi salama ya mtandao

Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji  Digital Agenda For Initiative Tanzania.
UN News
Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji Digital Agenda For Initiative Tanzania.

UN na harakati za usimamizi wa matumizi salama ya mtandao

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mivutano inaendelea ndani ya mikutano ya Umoja wa Mataifa ya kuweka  miongozo ya usalama na matumizi ya teknolojia  lakini hatimaye tutafikia muafaka ili tuwe na usimamizi mzuri wa usalama wa mtandao, amesema Peter Mmbando Mkurugenzi Mtendaji na Muasisi Digital Agenda For Tanzania Initiative.

Digital Agenda For Tanzania Initiative au DA4TI linajishughulisha na kutoa elimu na hamasa juu ya matumizi salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, TEHAMA wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unahaha kupata muongozo huo.

Ni lini vikao vilianza?

Harakati za kusaka mwongozo huo zilianzia mwaka 2020, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba 75/240, lilianzisha kikundi kazi kipya kikiwa na wajibu wa kuweka miongozo ya  usalama na matumizi ya TEHAMA.

Kikundi hicho kilichoanza mikutano yake mwaka 2021 kinatakiwa kukamilisha kazi mwaka 2025 ambapo mazungumzo yako chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa, yakihusisha nchi wanachama na mashirika ya kiraia.

Mtandao wawezesha vita kupiganwa ardhini na mtandaoni

Tarehe 4 hadi 8 mwezi huu wa Machi ulifanyika mkutano wa 7 na miongoni mwa walioshiriki ni Bwana Mmbando, ambaye katika mahojiano na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa alisema kuwa “mazungumzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani hivi sasa maisha yamebadilika. Maisha yako mtandaoni, watu wafanya kazi kimtandao na watu wasio na nia njema wanaingilia kati au wanadukua na kufanya uhalifu.”

Ameongeza kuwa hivi sasa vita inapiganwa kwa njia mbili yaani Hybrid, kimtandao na kwenye uwanja wa mapigano. “Pande zinahasimiana na kulalamikiana kuwa upande mmoja umedukua taarifa nyeti za miundombinu huku upande unaolalamikiwa unakataa.”

Wahalifu wanatumia vibaya mitandao

Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji  Digital Agenda For Initiative Tanzania.
UN News
Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji Digital Agenda For Initiative Tanzania.

Bwana Mmbando amesema pia kuna watu wanatumia mitandao kufanya wizi, kusambaza kauli za chuki na hata kuendeleza uonevu wa mtandaoni.

“Usalama wa kimtandao umetikiswa tangu kuibuka kwa janga la COVID-19 kwani huduma nyingi zilianza kufanyika kwa mtandao,” sasa maharamia wa mtandaoni wanatumia fursa kufanya uhalifu.

Amesema Akili Mnemba nayo imeongeza changamoto kwani baadhi ya watu wanaitumia vibaya.

Sasa mkutano unalenga kuweka mwongozo kuwe na usimamizi hivyo Umoja wa Mataifa ukaona bora mkutano huu ufanyike kwani maisha ya mtandaoni yanatumia takwimu au data nyingi na mtu anaweza kuzitumia vibaya.

“Zikitumika vizuri zinaleta maendeleo, mfano wakati wa sensa Tanzania tulifanya kidijitali, ilikuwa ni matumizi sahihi ya mtandao, lakini mtu mwingine anaweza kukiuka kanuni za matumizi na akazitumia vibaya ikaleta madhara,” amesema Mtendaji Mkuu huyo wa DA4TI.

Maslahi yasababisha kuweko kwa vuta nikuvute

Bwana Mmbando amesema kuna mvutano baina ya washiriki wa mkutano huo kwani kuna wanaodai kuweko na faragha, wengine uhuru wa kujieleza. Kuna wanaotaka uwajibikaji na uwazi lakini wengine hawapendi kwani utafichua mambo yao.

Alipoulizwa iwapo kuna matumaini ya mikutano hiyo inayopaswa kufikia ukomo mwakani 2025 kuzaa matunda, Bwana Mmbando amesema “tunahitaji tuwe na mashauriano na mwongozo  mzuri ili hatimaye tufikie muafaka. Na hii inatakiwa iwe endelevu ili hatimaye tupate vitu ambavyo hata vikikaa muda mrefu vinakuwa ni majawabu sahihi.”