Juhudi mpya za kukabili usafirishaji haramu wa binadamu

28 Machi 2018

Katika juhudi za kukabiliana ipasavyo usafirishaji haramu wa binadamu, Umoja wa Mataifa, kupitia shirika lake la kuhudumia wahamiaji, IOM na ofisi yake ya  kudhibiti madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC wamezindua juhudi mpya za pamoja za kukabiliana na uhalifu huo.

Katika uzinduzi  uliofanyika Vienna Austria, mkuu wa UNODC, Yury Fedotov, amesema kuwa ni lazima washirikiane kuwanyima  njia wahalifu, kwa minajili ya kulinda maisha  na usalama wa watu.

Juhudi hizo mpya zinahimiza  washikadau kuungana katika vita dhidi ya usafirishaji haramu wa watu.

Baadhi ya mbinu ni utafiti wa pamoja, kuzidisha uwezo wa mataifa wanachama katika vita hivyo na pia kuvunja mitandao ya wahalifu.

Mkurugenzi wa kikanda wa IOM, kanda za Kusini Mashariki, Mashariki mwa Ulaya pamoja na Asia ya kati, Argentina Szabados, amesema utashi wa kisiasa na sheria vipo bali kinachokosekana ni utekelezaji.

Ameongeza kuwa usafirishaji haramu wa watu kuvuka mipaka ya nchi ni kosa la jinai la kimataifa na kwa hivyo linahitaji ushirikiano wa kimataifa akiongeza kuwa wakati huu kunahitajika vitendo  kwani watu wengi wamepoteza maisha na wengine kupitia mateso  mengi.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud