Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya wiki kadhaa, hatimaye timu za misaada za UN zafika katika jiji la Gaza

Meli ya shirika la Open Arms ikiwa imesheheni chakula na maji na wafanyakazi waliojitolea tayari kusaidia walio hatarini zaidi huko Gaza.
© Open Arms
Meli ya shirika la Open Arms ikiwa imesheheni chakula na maji na wafanyakazi waliojitolea tayari kusaidia walio hatarini zaidi huko Gaza.

Baada ya wiki kadhaa, hatimaye timu za misaada za UN zafika katika jiji la Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Kwa mara ya kwanza baada ya wiki kadhaa, msaada wa kutosha watu 25,000 umefika katika Jiji la Gaza limesema shirika la Umoja wa Mataifa la  Mpango wa Chakula duniani WFP hii leo wakati wakitoa wito wa kuruhusiwa kuingia kwa misheni za misaada kila siku na ufikiaji bora huko Gaza.

"WFP iliwasilisha chakula cha kutosha watu 25,000 katika mji wa Gaza mapema Jumanne katika msafara wa kwanza uliofaulu kuelekea kaskazini tangu tarehe 20 mwezi Februari," Umesema ujumbe uliochapishwa na shirika hilo kupitia mtandao wake wa kijamii wa X. "Wakati wananchi wengi walioko Kaskazini mwa Gaza kuwa kwenye ukingo wa njaa, tunahitaji kuwa tunasafirisha misaada kila siku na tunahitaji maeneo ya kuingia moja kwa moja kaskazini."

Taarifa hiyo njema inakuwa wakati huu ambapo maafisa wa misaada wa Umoja wa Mataifa wamekaribisha taarifa ya kwamba meli ya misaada imeondoka Cyprus kuelekea Gaza ikiwa imebeba tani 200 za misaada lakini wamesisitiza kwamba msaada huo "sio mbadala" wa usaidizi wa nchi kavu kwa wakazi wa Gaza ambao kwa sasa wanakaribia kukumbwa na janga la njaa.

Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada, OCHA Jens Laerke akizungumzia meli hiyo amesema “Chakula chochote na usaidizi mwingine wa dharura unaokuja Gaza, kama tunavyojua sote, unahitajika sana; hakuna swali kuhusu hilo, kwahiyo inathaminiwa sana…Lakini si mbadala wa usafiri wa nchi kavu wa chakula na misaada mingine ya dharura hadi Gaza na hasa kaskazini mwa Gaza. Haiwezi kufidia hilo.”

Jaribio la usaidizi wa baharini

Maoni hayo ya afisa huyo wa Umoja wa Mataifa yanakuja wakati shirika la kimataifa la kutoa misaada la World Central Kitchen lilipotangaza kwamba meli yake, Open Arms, ilikuwa imeanza safari kuelekea Gaza, umbali wa maili 200 kutoka baharini. "Watu wa Kaskazini watapatiwa mlo!" ulisema ujumbe wa shirika hilo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter.)

Shirika hilo lisilo la kiserikali tayari limefanya kazi na timu za misaada za Umoja wa Mataifa huko Rafah kusini mwa Gaza, ambapo takriban watu milioni 1.5 wameenda kusaka hifadhi kutokana na mashambulizi ya kila siku ya Israel na mapigano kwa muda wa miezi mitano, yakichochewa na mashambulizi ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas nchini Israel na kusababisha vifo vya watu 1,200 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka.

Mikasi ya watoto yakataliwa 

Akisisitiza hali mbaya ya dharura ya kibinadamu ambayo bado inatokea huko Gaza, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, amelaani kukataliwa kuruhusu vitu vinavyoitwa "matumizi ya aina mbili" yanayokusudiwa kwa eneo hilo.

"Lori lililokuwa limepakia misaada limerudishwa kwa sababu lilikuwa na mikasi iliyotumika katika vifaa vya matibabu vya watoto," Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa UNRWA Jumanne ameandika kupitia mtandao wake wa X.

"Mikasi ya kimatibabu sasa imeongezwa kwenye orodha ndefu ya bidhaa zilizopigwa marufuku ambazo Mamlaka za Israeli zinaainisha kuwa 'kwa matumizi mawili'. Orodha hiyo inajumuisha vitu vya kimsingi na vya kuokoa maisha: kuanzia dawa ya usingizi, taa za jua, mitungi ya oksijeni na vipumuaji, hadi vidonge vya kusafisha maji, dawa za saratani na vifaa vya uzazi.

"Uondoaji wa vifaa vya kibinadamu na utoaji wa vitu vya kimsingi na muhimu unahitaji kuwezeshwa na kuharakishwa. Maisha ya watu milioni mbili yanategemea hilo, hakuna muda wa kupoteza.” Amesema Lazzarini. 

Chaguzi zote

Alipoulizwa na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi ikiwa Umoja wa Mataifa unaweza kutumia ukanda mpya wa baharini kati ya bandari ya kusini ya Larnaca huko Cyprus na Gaza, Bw. Laerke wa OCHA alijibu kwamba "njia zozote za kuingia Gaza zinapaswa kuangaliwa".

Lakini kufuatia kukataa mara kwa mara kwa mamlaka za Israeli kuruhusu misafara ya kibinadamu kufika kaskazini na hali zisizo salama kwa timu za misaada, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kwamba "tunahitaji ufikiaji wa njia ya ardhi na uwasilishaji salama na wa kawaida ndani ya Gaza pia".

Njaa 'imekaribia'

Katika hatua nyingine Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula dunaini WFP Cindy McCain ameonya hapo jana kwamba njaa "imekaribia" huko Gaza na itaepukwa tu ikiwa misaada ya kibinadamu itaongezeka "kwa kasi".

Akizungumza akiwa mjini Roma, Italia Mkurugenzi Mtendaji wa WFP alisisitiza wasiwasi mkubwa kwa watu "kote Gaza, hasa kaskazini, ambako iko katika hatari ya maafa ya kibinadamu.

"Kama hatutaongeza kwa kiasi kikubwa ukubwa wa misaada inayokwenda katika maeneo ya kaskazini, njaa iko karibu. Imekaribia.”

Afisa huyo mkongwe wa masuala ya misaada alieleza kuwa WFP ililazimika kusitisha utoaji wa misaada kaskazini mwa Gaza tarehe 20 Februari, 2024 kutokana na wasiwasi kuhusu "Usalama wa wafanyakazi wetu na kutokana na uvunjaji wa sheria na utaratibu".

Mkuu huyo wa WFP alisisitiza kwamba chaguzi zote zinachunguzwa ili kupunguza mzozo wa njaa kaskazini mwa Gaza, ikiwa ni pamoja na Msaada unaodondoshwa kwa njia ya hewa, lakini "hawatawahi kutoa kiasi kinachohitajika ambacho ufikiaji wa barabara unaweza".

Ufikiashaji wa misaada kwa njia ya barabara "na matumizi ya bandari zilizopo na vivuko ndiyo njia pekee ya kuingiza misaada Gaza kwa kiwango kinachohitajika sasa," mkuu wa WFP alisisitiza. "Tunahitaji lori 300 za chakula kuingia Gaza kila siku."