Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa Ramadhan tusitishe uhasama Gaza na Sudan: Guterres

Mamilioni ya watu kote ulimwenguni wanapoanza kuadhimisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwa huzuni huko Gaza na katika eneo lote, wengi wataadhimisha mwezi huu wakikabiliwa na migogoro, kufukuzwa na hofu.
© UNRWA
Mamilioni ya watu kote ulimwenguni wanapoanza kuadhimisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwa huzuni huko Gaza na katika eneo lote, wengi wataadhimisha mwezi huu wakikabiliwa na migogoro, kufukuzwa na hofu.

Ni wakati wa Ramadhan tusitishe uhasama Gaza na Sudan: Guterres

Amani na Usalama

Leo ni mwanzo wa mwezi mktukufu wa Ramadhan ambapo Waislamu kote duniani hudumisha na kuchagiza tunu za amani, maridhiano na mshikamano lakini uhasama unaendelea hususani sehemu mbalimbali duniani ikiwemo Gaza ambako mauaji , na mashambulizi hayajakoma amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani hii leo. 

“Mauaji, mabomu na umwagaji damu unaendelea huko Gaza hivyo ndivyo alivyoanza Katibu Mkuu katika tarifa yake fupi kwa waandishi wa habari akikumbusha kuwa ni hivi majuzi tuliingia mwezi wa sita tangu shambulio la kigaidi la Hamas nchini Israel na mashambulizi mabaya ya Israel huko Gaza.

Amesema leo ana ombi kubwa ambalo ni “kuheshimu dhamira ya Ramadhani kwa kunyamazisha mtutu wa bunduki na kuondoa vikwazo vyote ili kuhakikisha utoaji wa misaada ya kuokoa maisha kwa kasi na kiwango kikubwa kinachohitajika.”

Pia ametaka wakati huohuo kwa kuzingatia dhamira ya Ramadhani kuwaachilia mateka wote wanaoshikiliwa mara moja.

Dunia inakodolea macho kinachoendelea

Katibu Mkuu ameonya kwamba “Macho yadunia yanatazama. Macho ya historia yanatazama. Hatuwezi kuyapa kisogo yanayoendelea ni lazima tuchukue hatua kuepusha vifo vinavyoweza kuzuilika.”

Amesema dunia imeshuhudia mwezi baada ya mwezi mauaji ya raia na uharibifu wa miundombinu ya raia kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea katika miaka yangu yote akiwa Katibu Mkuu.

Na kwamba msaada wa kuokoa Maisha kwa raia Gaza unaingia kwa vikwazo vikbwa na wakati mwingine hauingii kabisa.

Amesema hivi sasa Sheria ya kimataifa za kibinadamu ziko katika hali mbaya.Na tishio la Israel kushambulia Rafah zinaweza kuwatumbukiza kuzimu zaidi watu wa Gaza.

Maombi ya familia za waathirika

Amesema pamoja na kwamba viongozi wa Dunia na wahudumu wa kibinadamu wamekuwa wakitoa wito wa kusitishwa mapigano wito mahsusi umetoka kwa familia za waathirika wa vita hivi.

Sitasahau mikutano yangu pamoja nao na wamesimama kwenye jukwaa hili na kukuhutubia wameungana kwa ujasiri mkubwa na maumivu yasiyopimika.

Familia za mateka wa Israeli ambao wameeleza mateso na uchungu wao na wameomba kuachiliwa mara moja kwa wapendwa wao.

Pia alikutana na familia za waathirika wa Gaza ambazi zimeomba uhasama kutishishwa mara moja “Kama mmoja wa wanafamilia hao alisema, Hatuko hapa kwa ajili ya rambirambi. Hatupo hapa kwa ajili ya kuomba msamaha. Tuko hapa kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za haraka. Je, hili ni kubwa sana kuliomba? Ni lazima tusikilize na kutii sauti hizo.” Amesesisitiza Guterres.

Wakimbizi wa Sudan katika kituo cha usafiri kinachosimamiwa na Umoja wa Mataifa huko Renk, Sudan Kusini.
© IOM/Elijah Elaigwu
Wakimbizi wa Sudan katika kituo cha usafiri kinachosimamiwa na Umoja wa Mataifa huko Renk, Sudan Kusini.

Usitishaji uhasama Sudan

Pia Katibu Mkuu ametoa ombi kwa ajili ya Sudan akisema “Leo, pia ninawasilisha ombi langu la kusitishwa kwa uhasama nchini Sudan katika wakati huu wa Ramadhani.”

Ameendelea kusema kuwa mapigano huko lazima yakome kwa ajili ya watu wa Sudan ambao wanakabiliwa na njaa, vitisho na shida zisizoelezeka.

Amesisitiza kuwa “Huko Gaza, Sudan, na kwingineko, huu ni wakati wa kuleta amani.

Kisha akawageukiwa viongozi na kusema “Natoa wito kwa viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii kila mahali kufanya kila wawezalo ili kufanya kipindi hiki kitakatifu kuwa wakati wa huruma, vitendo mema  na amani.”

Amekumbusha kwamba zaidi ya Ramadhani, Wakristo hivi karibuni wataadhimisha Pasaka na Wayahudi wataadhimisha Passover “Ni wakati wa kumaliza mateso ya kutisha na wakati wa kufanya hivyo ni sasa.”