Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Nchini Jordan wakimbizi wakiwa pamoja kwa futari wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kila la heri Waislam wote na Ramadhani njema: Guterres

© UNHCR/Benoit Almeras
Nchini Jordan wakimbizi wakiwa pamoja kwa futari wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kila la heri Waislam wote na Ramadhani njema: Guterres

Amani na Usalama

Mwezi mtukufu wa Ramadhan umewadia na Waislam kote duniani wanaanza mfungo.  

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akishikamana nao amewatakia heri na baraka kupitia ujumbe maalum akisema “Natuma salamu zangu za dhati wakati mamilioni ya Waislamu duniani kote wakianza mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hiki ni kipindi cha huruma na Imani, ni wakati wa kutafakari na kujifunza na ni fursa ya kuja pamoja na kuinuana.” 

Guterres amekumbusha kuwa alipokuwa kamishna mkuu wa wakimbizi, alianza mazoea ambayo anayaendeleza kwa fahari kama Katibu Mkuu. 

“Kila Ramadhani, nilipata heshima ya kutembelea nchi za Kiislamu, kufunga kwa mshikamano na kushiriki futari na watu. Kwa bahati mbaya, janga la COVID-19 lilifanya hilo lisiwezekane, lakini nina furaha kuanza tena utamaduni huu mwaka huu.” 

Ameongeza kuwa katika nyakati hizi za majanga na mateso, fikra na moyo wake viko kwa kila mtu anayekabiliwa na migogoro, kulazimika kuhama na hofu. 

“Quran tukufu inatufundisha kwamba Mungu aliumba mataifa na makabila ili tujuane. Katika mwezi huu mtukufu na kila siku, tuchukue msukumo kwa kufanya kazi bega kwa bega kwa ajili ya usalama, utu na ustawi wa wanawake na wanaume wote. Tujifunze kutoka kwa kila mmoja na, kwa pamoja, ili tujenge ulimwengu wa amani. Ramadhani Kareem.”