Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Tuwekeze zaidi katika wanawake ili kutokomeza mfumo dume

Wanawake wakulimawakivuna mboga kaskazini mashariki mwa Guinea.
© WFP/Studio 2k
Wanawake wakulimawakivuna mboga kaskazini mashariki mwa Guinea.

Guterres: Tuwekeze zaidi katika wanawake ili kutokomeza mfumo dume

Wanawake

Katika kusherehekea siku ya wanawake duniani kote Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewapongeza wanawake na wasichana kwa kupata mafanikio makubwa na kuondoa vikwazo, kuvunja fikra potofu na kuchochea maendeleo kuelekea dunia yenye haki na usawa zaidi.  

Katika ujumbe wake kwa siku hii Katibu Mkuu Guterres amesema “Pamoja na juhudi wanazozifanya kila siku bado wanakabiliwa na vikwazo vikubwa. Mabilioni ya wanawake na wasichana wanakabiliwa na kuenguliwa, ukosefu wa haki na ubaguzi, ilhali janga lililojikita la ukatili dhidi ya wanawake lilikimomonyoa ubinamu.”

Amesema ni vyema kuongeza juhudi ikiwemo za kisheria katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake kwani kwa kasi ya sasa itachukua miaka miatatu kupata usawa.

Akieleza nini kifanyike amesema “ tunapaswa kuwekeza kwenye miradi ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na kuchochea ujumuishaji wanawake na uongozi wa wanawake kwenye uchumi, teknolojia za kidijitali, ujenzi wa amani na hatua kwa tabianchi.Yote hii inategemea kupatikana kwa fedha kwa ajili ya maendeleo endelevu ili nchi ziwe na fedha za kuwekeza kwa wanawake na wasichana.”

Kauli mbiu ya siku ya wanawake kwa mwaka huu ni wekeza kwa wanawake ili kuharakisha maendeleo na Mkuu huyo wa umoja wa Mataifa amesema inatukumbusha kuwa kutokomeza mfumo dume kunahitaji kuweko kwa fedha mezani.

“Tunahitaji pia kuongeza idadi ya wanawake viongozi kwenye sekta ya biashara, Benki Kuu na Wizara za Fedha. Hii inaweza kusaidia kuchochea uwekezaji kwenye sera na miradi inayokidhi mahitaji ya wanawake na wasichana.

Haki za wanawake zimedhihirisha kuwa njia ya haki ya jamii zenye haki, amani na ustawi. Hii ni vema kwetu sote. 

“Kwa Pamoja, hebu na tuchukue hatua za haraka kufanya kuwa halisia.”

Usawa kwa wote

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women linaadhimisha siku hii kwa kufanya mkutano mkubwa katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani utakao wakutanisha pamoja viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa masuala ya wanawake. 

UN Women wamesema katika mwaka huu ambapo karibu nusu ya watu duniani wanaishi katika nchi zinazoshiriki katika uchaguzi, Siku hii ya Kimataifa ya Wanawake ni fursa muhimu ya kufafanua siku zijazo tunazotaka.

Wakati mizozo, mabadiliko ya tabianchi na jamii zenye mgawanyiko zikididimiza miongo kadhaa ya maendeleo katika usawa wa kijinsia, UN Women inatoa wito waku "Wekeza kwa wanawake ili Kuharakisha Maendeleo" ili hatimae dunia iweze kufikia faida ya usawa wa kijinsia kwa wote.