Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM: Mwaka 2023 takriban wahamiaji 8,600 wamepoteza maisha

Ajali kubwa zaidi ya meli kuwahi kutokea katika historia ya Ugiriki imesababisha vifo vya mamia ya watu. (Maktaba)
IOM/Amanda Nero
Ajali kubwa zaidi ya meli kuwahi kutokea katika historia ya Ugiriki imesababisha vifo vya mamia ya watu. (Maktaba)

IOM: Mwaka 2023 takriban wahamiaji 8,600 wamepoteza maisha

Wahamiaji na Wakimbizi

Mwaka 2023 takriban wahamiaji 8,565 wamekufa wakati wakiwa njiani Kwenda kusaka maisha nchi nyingine ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 ya vifo ikilinganishwa na mwaka 2022 na kufanya mwaka 2023 kuwa mwaka mbaya zaidi kwenye rekodi za Shirika la Umoja wa Mataifa la wahamiaji IOM. 

IOM kupitia mradi wa wahamiaji waliopotea ambao unahusika na kukusanya takwimu za wahamiaji waliopotea na kufariki na kuziweka wazi kwa umma tangu mwaka 2014 umeeleza hitaji la dharura la kuchukua hatua ili kuzuia watu wengi zaidi kupoteza maisha.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM Ugochi Daniel katika taarifa yake kutoka Geneva Uswisi na Berlina Ujerumani amesema “Tunavyoadhimisha miaka 10 ya mradi wa wahamiaji waliopotea kwanza tunawakumbuka wale wote waliopoteza maisha. Kila kifo cha mtu mmoja ni janga baya la kibinadamu ambalo hujirudia kupitia familia na jamii kwa miaka mingi ijayo,”

Daniel ameongeza kuwa “Takwimu hizo za kutisha zinazokusanywa na mradi wa wahamiaji waliopotea ni ukumbusho kwamba lazima tujitolee tena kuchukua hatua kubwa zaidi ambazo zinaweza kuhakikisha kuna uhamiaji salama kwa wote, ili miaka 10 kutoka sasa, watu wasihatarishe maisha yao kutafuta maisha bora zaidi.”

Takwimu za kikanda

Njia ya Mediterania ndio imeendelea kuwa njia mbaya zaidi kwa wahamiaji kwenye rekodi za IOM ambapo angalau vifo 3,129 na watu kupotea vimeripotiwa. Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya vifo vilivyorekodiwa katika Mediterania tangu mwaka 2017.

Kikanda, idadi isiyokuwa ya kawaida ya vifo vya wahamiaji ilirekodiwa kote Barani Afrika (1,866) na Barani Asia (2,138). 

Barani Afrika, vifo vingi vilitokea katika Jangwa la Sahara na njia ya bahari kuelekea Visiwa vya Canary. 

Huko Asia, mamia ya vifo vya wakimbizi wa Afghanistan na Rohingya wanaokimbia nchi zao zilirekodiwa mwaka jana.

Mradi wa wahamiaji waliopotea

Ukiwa unatimiza mwaka wake wa kumi tangu kuanzishwa kwake, mradi huu wa Wahamiaji Waliopotea kama hifadhidata pekee ya wazi ya vifo na wahamiaji waliopotea umerekodi zaidi ya watu 63,000 ulimwenguni. 

Hata hivyo kwa mujibu wa IOM idadi ya kweli inakadiriwa kuwa ya juu zaidi kutokana na changamoto katika ukusanyaji wa takwimu hasa katika maeneo ya mbali kama vile Mbuga ya Kitaifa ya Darien huko Panama na kwenye njia za baharini, ambapo IOM hurekodi mara kwa mara ripoti za ajali zisizoonekana za meli ambapo boti hutoweka bila kuonekana.

Ripoti hizi zinazotolewa na mradi huu zinasaidia IOM na wadau kutathmini kazi inayoendelea ya kupanua wigo wa njia salama na za kawaida za kutumika kwa uhamiaji, kuimarisha shughuli za utafutaji na uokoaji, na kusaidia watu binafsi na familia zilizoathirika. 

IOM, pamoja na mashirika mengine mengi, na kama Mratibu wa Mtandao wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhamiaji, inatoa wito kwa serikali na jumuiya ya kimataifa kuendelea kufanya kazi pamoja ili kuzuia kupoteza maisha zaidi na kudumisha utu na haki za watu wote.