Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambi ya wakimbizi ya Rohingya yateketea kwa moto

Moto katika kambi ya 5 ya wakimbizi wa Rohingya ulianza mapema asubuhi ya 7 Januari 2024.
© UNICEF/Salim Khan
Moto katika kambi ya 5 ya wakimbizi wa Rohingya ulianza mapema asubuhi ya 7 Januari 2024.

Kambi ya wakimbizi ya Rohingya yateketea kwa moto

Msaada wa Kibinadamu

Mnamo saa 1 asubuhi siku ya tarehe tarehe 7 Januari mwaka 2024, moto mkubwa ulizuka katika Kambi ya 5 ya wakimbizi ya Rohingya nchini Bangladesh.

Moto huo umesababisha zaidi ya wakimbizi 5,000 ikiwa ni pamoja na watoto 3,500 kupoteza makazi yao.

Jumla ya makazi 842 yaliathirika, pamoja na makazi 749 yaliyoharibiwa kabisa na moto na 93 kuharibiwa kidogo.

Vituo vya jumuiya 33 viliharibiwa ikiwa ni pamoja na vituo vya afya, vituo vya kujifunzia, misikiti na kituo cha kuzima moto kinachohamishika.

Ingawa hakuna vifo vilivyoripotiwa, angalau watoto 1,500 walipoteza fursa ya kupata elimu wakati maeneo yao 20 ya kujifunzia  yameharibiwa na moto.

Wakati tathmini ya athari za moto huo ikiendelea ili kubaini kiwango kamili cha uharibifu, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na washirika wake wameeleza watajenga mahema ya muda ili kuwawezesha watoto kujifunza huku madarasa yakijengwa upya.

Katika taarifa iliyotolewa na Mwakilishi wa UNICEF nchini Bangladesh, Sheldon Yett, amesema, “UNICEF na washirika wake wanafanya kazi usiku kucha ili kulinda na kusaidia watoto waliopata kiwewe na familia zao. Tukumbuke, watoto hawa tayari wameepuka ukatili na kiwewe. Kwa hivyo, kuna umuhimu wa haraka wa kufanya kazi kwa karibu na mamlaka za mitaa, mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine ili kuwapa walio hatarini zaidi makazi na kujibu mahitaji yao ya kimsingi ili watoto wote walioathiriwa wawe salama, wenye afya na kulindwa”