Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO inawasaidia wakimbizi wanaokimbia machafuko nchini DRC kupata huduma za matibabu

Wakimbizi wa ndani katika kambia ya wakimbizi ya Bulengo nchini DR Congo. .
UN News/Byobe Malenga
Wakimbizi wa ndani katika kambia ya wakimbizi ya Bulengo nchini DR Congo. .

WHO inawasaidia wakimbizi wanaokimbia machafuko nchini DRC kupata huduma za matibabu

Afya

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia kongo DRC Jimboni kivu kaskazini zaidi ya wakimbizi milioni 2.5 wanaishi katika kambi za wakimbizi ambazo zina hali mbaya ambayo ni tishio kwa afya zao. Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO linatoa usaidizi kwa wakimbizi hao.  

Kambi ya wakimbizi ya Bulengo iliyoko jimboni kivu kaskazini, Video ya WHO inaonesha maelfu ya mahema meupe chini udongo mweusi wa mfinyazi, mamia ya watu wanaenda huku na kule ndani ya kambi hiyo. 

WHO inahofia mlundikano huu wa wakimbizi kuleta mlipuko wa magonjwa kama Malaria, magonjwa ya kupumua, ya kuhara na mengine ya kuambukiza. WHO ikishirikiana na wadau wengine wameanzisha vituo vya afya na wagonjwa wanafika kupata huduma, mmoja wao ni Desange Ndamwenge na mwanae.  

“Nimemleta mtoto wangu hapa asubuhi kwa ajili ya matibabu na ili tupate dawa. Mtoto ana mwaka mmoja na nimgonjwa sana ndio maana nimemleta hapa. Na mimi pia ni mgonjwa. Tumepata dawa wameshatupatia dawa za maji.”

Aubedi Dunia Sebirayi ni nesi mkuu katika kambi ya Bulengo na anasema 

“Hapa tunatoa huduma ya afya ya msingi, wakimbizi hawa wanapokuja na ninwagonjwa hawana hela ya kwenda hospitali kupata matibabu. Tunatoa huduma bure, kwa siku tunaona wagonjwa kati ya 80 mpaka 120 na kati yao unakuta wagonjwa wawili au watatu tunawapeleka katika hospitali.”

Kwa mujibu wa Meneja wa Matukio wa WHO nchini DRC Dkt. Guy Kalambayi wakimbizi hao wa ndani wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiafya lakini kwa kuwapatia dawa, kutoa huduma za kujifungua, kutoa chanjo, na kutibu kipindupindu wanazuia vifo vingi sana na kuokoa maisha. 

Takwimu za WHO zinaonesha kwa wastani tangu mwezi Februari 2023 kwa mwezi wanawake 100 wanajifungua na hakuna kifo cha mjamzito hata mmoja tangu wameanza kutoa huduma. Kavira Mwaliweka ni mkunga katika kituo cha afya ya Bulengo 

“Kama tusingekuwa na wodi hii ya kujifungulia hapa Bulengo tungekuwa na vifo vingi sana vya wajawazito kwasababu kambi hii iko mbali sana na kituo cha afya. Tunajisika kuwa na bahati sana kwa kutokuwa na kifo hata kimoja cha mjamzito.”

Elise ni mmoja ya wajawazito waliojifungua salama na sasa anarejea nyumbani kambini na mwanaye kwa furaha.