Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO: Hatua za haraka zinahitaji kufikia wenye uhitaji nchini Sudan

Mwanamke akipokea matibabu katika kituo cha matibabu ya kipindupindu nchini Sudan.
© WHO/Ala Kheir
Mwanamke akipokea matibabu katika kituo cha matibabu ya kipindupindu nchini Sudan.

WHO: Hatua za haraka zinahitaji kufikia wenye uhitaji nchini Sudan

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutetea upatikanaji wa haraka na bila vikwazo wa huduma za afya ili kuokoa maisha ya wananchi wa Sudan na kuongeza haraka usambazaji wa misaada ili kushughulikia mahitaji ya dharura ya watu walio katika hatari zaidi.

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na WHO kanda ya mashariki mwa mediterania imesema ikiwa ni takriban miezi 10 tangu kuvuka kwa mzozo nchini Sudan takriban watu million 8 nchini humo wamefurushwa makwao, milioni 6 wakiwa wakimbizi wa ndani na zaidi ya milioni 1.8 wakisaka hifadhi katika nchi Jirani. 

Waomba fedha ili kufikisha huduma

Kwa mujibu wa mpango wa mahitaji ya kibinadamu nchini Sudan kwa mwaka huu wa 2024 takriban watu milioni 15 wanahitaji usaidizi wa dharura wa afya lakini kutokana na changamoto za usalama na ufinyu wa rasilimali ni theluthi moja tu watu wenye uhitaji (watu milioni 4.9) ndio wamelengwa kufikiwa na huduma za afya. 

Kundi la Afya, linaloongozwa na WHO, linahitaji wadau kukidhi asilimia 100 ya mahitaji ya kifedha kwa ombi lao la dola milioni 178, ili waweze kukidhi mahitaji ya kiafya ya walengwa walio hatarini zaidi.

Mzozo huo umeleta athari si tu kwa nchi hiyo bali pia nchi Jirani zilizowapokea wakimbizi kutoka Sudan na kuongeza wasiwasi mkubwa wa milipuko ya magonjwa kutokana na watu kufurika huku kukiwa na uhaba wa maji safi na salama pamoja na huduma nyingine za kimsingi za kiafya za kuokoa maisha. 

WHO imesema changamoto ya kiafya nchini Sudan inazidishwa kuzorota kutokana na ukosefu wa uhakika wa chakula ambapo watu milioni 18 sawa na asilimia 37 wakiwa hawana uhakika wa chakula. 

Huduma finyu za matibabu

Ufikiaji wa huduma muhmu za afya umekuwa wa taabu kwani asilimia 70-80 ya vituo vya afya havifikiki au havifanyi kazi. Hali hii imeweka mzigo mkubwa kwa vituo vilivyosalia vinavyofanya kazi kutokana na idadi kubwa ya watu wanaosaka huduma za matibabu. 

Watu wanakufa kwa kukosa huduma muhimu za afya na dawa kwa utapiamlo mkali au kutibu magonjwa sugu kama shinikizo la damu, kisukari, figo na saratani. Wanawake wajawawazito na watoto wapo kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa na kufa kutokana na huduma za mama na mtoto kuathirika vibaya ikiwemo ukosefu wa chanjo kwa watoto. 

Utapiamlo mkali unaweza kuwa na madhara ya muda mrefu na kuathiri afya kwa jamii. Wananchi pia wanaathirika na vifo na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na surau.

Tangu mlipuko unaoendelea wa kipindupindu kutangazwa mwezi Septemba 2023, majimbo 11 kati ya 18 ya Sudan yameripoti kuwa na wagonjwa wa kipindupindu, huku wagonjwa 10,500 wakisajiliwa na vifo 300 vikirekodiwa mpaka kufikia mwezi Januari 31, 2024. Wakati idadi ya wagonjwa ikiendelea kupungua, idadi halisi ya wagonjwa kesi na vifo inaweza kuwa ya juu zaidi, kwani usahihi wa mfumo wa ufuatiliaji unaathiriwa na mapungufu ya ufikiaji wa watu.

WHO imeeleza pia inapanua uwezo wa shughuli zake kuvuka mpaka ili kutoa msaada muhimu kwa wadau wanaofanya kazi katika maeneo yasiyofikika na magumu kufikiwa.