Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande zote kwenye mzozo wa Gaza zinaweza kuwa zimefanya uhalifu wa kivita - Türk

Kitongoji cha Al-Shaboura huko Rafah, kimebaki magofu.
UN News/Ziad Taleb
Kitongoji cha Al-Shaboura huko Rafah, kimebaki magofu.

Pande zote kwenye mzozo wa Gaza zinaweza kuwa zimefanya uhalifu wa kivita - Türk

Amani na Usalama

Pande zote katika mzozo wa Gaza zimehusika na "ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu ikiwa ni pamoja na uwezekano wa uhalifu wa kivita", amesema afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu, Volker Türk.

Katika ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi yake kuhusu hali ya eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu iliyopangwa kuwasilishwa kwa Baraza la Haki za Kibinadamu baadaye hii leo, Kamishna Türk anarudia kulaani mauaji yaliyoongozwa na Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba 2023 ambayo yalisababisha takriban watu 1,200 kuuawa na kutaka kuachiliwa mara moja kwa mateka wote wa Israel.

Mtazamo wa hali mbaya

Kamishna Mkuu huyo wa Haki za Kibinadamu pia anasisitiza jinsi "kujibu mashambulizi  kwa kiasi kikubwa kulikofanywa na jeshi la Israeli kulivyosababisha "uharibifu na mateso yasiyokuwa ya kawaida" ambayo yamesababisha mzozo mbaya wa kibinadamu kustahimiliwa na Wananchi wa Gaza wanaokabiliwa na hali ya njaa.

"Ukiukwaji wa wazi wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa uhalifu wa kivita, umefanywa na pande zote," ripoti kutoka Ofisi ya Kamishna Mkuu inasema, kabla ya kutaka uchunguzi zaidi kubaini uwajibikaji na kuondokana na "kutokujali".

Wito wa kutendewa kibinadamu

Miongoni mwa hatua zinazotarajiwa kwa pande zinazopigana, kutoka kwenye ripoti ya mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa inayataka makundi yenye silaha ya Palestina huko Gaza "kuhakikisha watu wanatendewa kibinadamu na kuachiliwa mara moja kwa mateka wote", kuacha kurusha "makombora yasiyobagua" dhidi ya Israeli na kuwaondoa wapiganaji kutoka kwa majengo yanayotumiwa na raia.

Ripoti ya Kamishna Mkuu pia inatoa wito kwa Israel "kukomesha mara moja vitendo vyote vya adhabu ya pamoja" ya Wagaza ikiwa ni pamoja na "kuwazingira" na kuhakikisha "upatikanaji wa haraka wa bidhaa za kibinadamu na za kibiashara kote Ukanda wa Gaza, kulingana na mahitaji makubwa ya kibinadamu".

Akitoa wito kwa jeshi la Israel, Kamishna Türk anahimiza kurejeshwa kwa Wapalestina wote walioondolewa katika makazi yao na vita, pamoja na kufuata sheria za kimataifa za kibinadamu kwa kukomesha matumizi ya silaha za milipuko "pamoja na athari za eneo kubwa" katika maeneo yaliyojengwa. 

Ulinzi lazima pia utolewe kwa hospitali na miundombinu mingine ya kiraia ambayo ni muhimu kwa maisha ya watu, ripoti hiyo inasema.