Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa chakula wa dharura kutoka Ukraine wawasili Sudan: WFP

Msaada wa dharura wa chakula kutoka Ukraine wawasili Sudan, nchi iliyokumbwa na vita.
© WFP/Abubaker Garelnabei
Msaada wa dharura wa chakula kutoka Ukraine wawasili Sudan, nchi iliyokumbwa na vita.

Msaada wa chakula wa dharura kutoka Ukraine wawasili Sudan: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Msaada wa chakula cha dharura uliotolewa na Ukraine kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP kwa ajili ya operesheni zake nchini Sudan, leo umewasili katika bandari ya Port Sudan na kuapakiwa Kwenye malori tayari kwa kuwasambazia watu wenye uhitaji wa haraka.

Ama kwa hakika wahenga hawakukosea kusema kutoa ni moyo , kwani kwa mujibu wa WFP Ukraine ambayo yenyewe iko katikati ya vita bado imeona umuhimu wa kuwasaidia wenye uhitaji zaidi kwa kuipa WFP ngano ambayo shirika hilo linasema itatosheleza kutoa mgao wa chakula wa mwezi mmoja kwa waathirika wa vita ndani ya Sudan.

Kuwasili kwa shehena hiyo ambayo ni sehemu ya mradi wa kibinadamu wa nafaka uliozinduliwa na Rais Zelensky wa Ukraine kumefanikishwa na serikali ya Ujerumani iliyolipia gharama zote ambazo ni Euro milioni 15 sawa na takriban dola milioni 16.2.

Vita ikishika kasi Sudan WFP inasema mahitaji ya kibinadamu na hasa chkula yanaongezeka kwa kasi pia. 

Kwa mujibu wa Eddie Rowe mkurugenzi wa WFP nchini Sudan "Hali ya kibinadamu nchini Sudan ni janga lakini tunahitaji kuchukua hatua sasa ili kuizuia kuendelea kuwa mbaya zaidi. WFP inafanya kazi kwa kasi kuweza kufikisha msaada wa chakula mikononi mwa familia zinazohitaji msaada huo haraka iwezekanavyo.”

Msaada wa dharura wa chakula kutoka Ukraine wawasili Sudan, nchi iliyokumbwa na vita.
© WFP/Abubaker Garelnabei
Msaada wa dharura wa chakula kutoka Ukraine wawasili Sudan, nchi iliyokumbwa na vita.

WFP inasema msaada wa ngano hiyo ambao ni tani 7,600 utagawanywa kwa familia ambazo nyingi zimefurushwa makwao kutokana na mapigano yanayoendelea na zinahaha kila uchao kuweka mlo mezani.

Rowe amesema msaada huu umewasili wakati muafaka kwani mapigano yakiendelea mgogoro wa njaa nchini Sudan unajongea hasa kabla ya msimu wa muambo mwezi Mei, wakati chakula kinakuwa haba, na njaa inaongezeka.

Amemalizia kwa kusema kuwa "Msaada huu utaiwezesha WFP kusaidia watu ambao maisha yao yamepinduliwa kabisa na vita. Tunaishukuru sana Ukraine na Ujerumani kwa kuwasaidia watu wa Sudan katika wakati ambao uhitaji ni mkubwa.”