Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Duniani kote kati ya kila watu 6 mtu 1 ameathiriwa na utasa au ugumba

Shirika la Afya Duniani linachukulia utasa kuwa suala la afya ya umma duniani.
© Unsplash/Jan Antonin Kolar
Shirika la Afya Duniani linachukulia utasa kuwa suala la afya ya umma duniani.

Duniani kote kati ya kila watu 6 mtu 1 ameathiriwa na utasa au ugumba

Afya

Idadi kubwa ya watu wameathiriwa na utasa au ugumba kwenye maisha yao, imeeleza ripoti mpya iliyochapishwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO.

Taarifa iliyotolewa na WHO kutoka jijini Geneva Uswisi imeeleza kuwa takriban 17.5% ya watu wazima, kiwango ambacho ni sawa na mtu 1 kati ya 6 ulimwenguni wameshindwa kuwa na uwezo wa kuzaa  yaani wana matatizo ya Utasa au ugumba, ikionesha hitaji la dharura la kuongeza ufikiaji wa huduma ya afya ya uzazi kwa gharama nafuu na huduma bora zaidi kwa wenye uhitaji.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, "Idadi kubwa ya watu walioathiriwa inaonyesha hitaji la kupanua wigo wa ufikiaji wa huduma ya uzazi na kuhakikisha suala hili haliwekwi kando tena katika utafiti wa afya na katika sera, ili njia salama, bora na za gharama nafuu za kupata uzazi zipatikane kwa wale wanaotafuta.”

Makadirio mapya yanaonesha tofauti ndogo katika kuenea kwa matatizo ya utasa au ugumba kati ya kanda. Viwango hivyo vinalinganisha nchi zenye kipato cha juu, cha kati na cha chini, na kuthibitisha kuwa hii ni changamoto kubwa ya kiafya duniani kote.

Kiwango cha maisha kilikuwa 17.8% katika nchi za kipato cha juu, na 16.5% katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Utasa ni nini?

Utasa au pia unafahamika kama ugumba, ni ugonjwa wa mfumo wa uzazi wa mwanamume au mwanamke, unaofafanuliwa kwa kushindwa kupata ujauzito baada ya miezi 12 au zaidi ya kujamiiana mara kwa mara bila kinga.

Hali hii inaweza kusababisha dhiki kubwa, unyanyapaa, na ugumu wa kifedha, na kuathiri ustawi wa kiakili na kisaikolojia wa watu.

Licha ya ukubwa wa suala hili, suluhu za uzuiaji, utambuzi na matibabu ya utasa bado hazifadhiliwi na hazipatikani na wengi kutokana na gharama kubwa, unyanyapaa wa kijamii na upatikanaji mdogo.

"Mamilioni ya watu wanakabiliwa na janga la gharama za huduma za afya baada ya kutafuta matibabu ya utasa, na kufanya hili kuwa suala kuu la usawa na mara nyingi huwa ni mtego wa umaskini wa matibabu kwa walioathirika," Amesema Dkt. Pascale Allotey, ,mkurugenzi wa Afya ya jinsi, Uzazi na Utafiti wa WHO, ambaye pia anahusika na Mpango Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Utafiti, Maendeleo na Mafunzo ya Utafiti katika Uzazi wa Binadamu (HRP).

Kwa sasa, katika nchi nyingi, matibabu ya uzazi yanafadhiliwa kwa kiasi kikubwa nje ya mfuko na hili mara nyingi husababisha gharama kubwa za kifedha.

Watu katika nchi maskini zaidi wanatumia sehemu kubwa ya mapato yao katika huduma ya uzazi ikilinganishwa na watu katika nchi tajiri. Gharama kubwa mara kwa mara huzuia watu kupata matibabu ya utasa au vinginevyo, inaweza kuwaingiza katika umaskini kama matokeo ya kutafuta huduma.