Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutumie sauti za manusura wa FGM kutokomeza kitendo hiki dhalili - Guterres

Wasichana waliokimbia makazi yao wanahudhuria warsha ya kuongeza uelewa dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na FGM huko Kosti, Sudan.
© UNICEF/Sara Awad
Wasichana waliokimbia makazi yao wanahudhuria warsha ya kuongeza uelewa dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na FGM huko Kosti, Sudan.

Tutumie sauti za manusura wa FGM kutokomeza kitendo hiki dhalili - Guterres

Afya

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake na watoto aw kike, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwenye ujumbe wake amesema mwaka huu wa 2024 wasichana milioni 4.4 wakiwa hatarini kukeketwa kila mtu achukue hatua maradufu kuepusha kitendo hicho ambacho kinakiuka haki za msingi wa binadamu na kusababisha machungu ya afya ya mwili na akili kwa wanawake na wasichana.

Ujumbe wa mwaka huu ni Sauti yake. Mustakabali wake. Wekeza katika harakati zinazosongeshwa na  manusura ili kutokomeza FGM. 

Ni kwa kuzingatia maudhui hayo ya mwaka huu, Guterres amesema inahitaji hatua za kimsingi kushughulikia maadili ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yanayosongesha ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana na kuzuia ustawi wao kielimu na kwenye ajira. 

“FGM ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaosababisha machungu kwenye maisha yote ya wanawake na wasichana waliokeketwa, machungu ya kiafya ya mwili na akili,” amesema Katibu Mkuu. 

Watoto wanahudhuria kikao cha uhamasishaji kuhusu FGM huko Katiola, Côte d'Ivoire.
© UNICEF/Olivier Asselin
Watoto wanahudhuria kikao cha uhamasishaji kuhusu FGM huko Katiola, Côte d'Ivoire.

Amesema harakati zozote za kutatua na kutokomeza janga hilo la ukeketaji lazima zianze na kuhoji mifumo dume na mitazamo ambayo ndio msingi wa kitendo hicho kinachochukiza. 

“Tunahitaji uwekezaji wa dharura na haraka wa kufikia malengo yaliyowekwa na Malengo ya MAendeleo Endelevu, SDGs ya kutokomeza FGM ifikapo mwaka 2023,” amesisitiza Guterres. 

Hivyo amesema “tunahitaji kupaza sauti za manusura na kusaidia juhudi zao za kudai maisha yao, kwa kuzingatia maumbo ya miili yao.”