Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Virusi vya Corona; nchi za Afrika Mashariki zimejiandaa- WHO

Hapa ni nchini China, mhudumu akiacha kifurushi nje ya nyumba kwa kuwa hawaruhusiwi kuingia kwenye majengo kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona nchini humo.
Man Yi
Hapa ni nchini China, mhudumu akiacha kifurushi nje ya nyumba kwa kuwa hawaruhusiwi kuingia kwenye majengo kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona nchini humo.

Virusi vya Corona; nchi za Afrika Mashariki zimejiandaa- WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika Mashariki, limesema kuwa mataifa ya ukanda huo yamejiandaa kudhibiti mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 wakati huu ambapo imeelezwa kwa mara ya kwanza kuna idadi kubwa ya visa vipya nje ya China.

Afisa wa kisayansi wa WHO kwa nchi za Afrika Mashariki, Dkt. Peter Borus aliyeko Nairobi Kenya, amesema hayo  katika mahojiano yake kwa njia ya simu na Flora Nducha wa UN News Kiswahili.

Dkt. Borus amesema “kwa maandalizi kuna vifaa na serikali ikiwa inaongoza kwa hii juhudi inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo WHO.”

Alipoulizwa iwapo maandalizi hayo kwa Kenya na nchi nyingine za Afrika Mashariki yanatosha, afisa huyo amesema kuwa, “kwa kikubwa ndio, wazi lazima kuwe na changamoto hapa na pale. Lakini nchi wamejitayarisha kabisa, ukiona vile wanafanya kazi kwenye viwanja vya ndege na bandarini Mombasa na kwingineko ambako watu wanaweza kujitokezea na hizo dalili za virusi hivyo. unaona kabisa nchi imejitayarisha hata leo tulikuwa kwenye maandalizi na wizara na washika dau wengine, hiki kikitokea nini kitafanyika,wagonjwa watapelekwa wapi,   jamii waelimishwa vipi, iko tayari.”

Dkt. Borus akaulizwa nini wito wake kwa jamii Afrika Mashariki ambapo amesema kuwa, “kwa umma wa Kenya na Afrika MAshariki, kitu cha muhmu ni kuhakikisha kwamba  kama kuna wasafiri wameingia kwa nchi, tungependa mwananchi na kila mmoja atoe taarifa kwa wafanyakazi wa Wizara ya Afya kwa kuwa ni muhimu sana habari zifikie Wizara ya Afya ili uchunguzi ufanyike na kubaini iwapo ni ugonjwa huo.

Na vipi hofu kwa wananchi kutoka mitandao ya kijamii? Afisa huyo wa kisayansi wa WHO amesema kuwa, “wananchi wasiwe na hofu , unajua wakati mwingine kwenye mitandao ya kijamii habari zingine zinakuwa si sahihi. Ningependa kusema kuwa habari ya kweli inatoka serikalini.”

Virusi vya Corona viliibuka nchini China na kutangazwa kuwa dharura ya afya ya umma duniani tarehe 30 mwezi uliopita wa Januari.