Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 400,000 watawanywa na kimbunga Freddy Madagascar na Msumbiji: IOM

Watoto wakiwa wamesimama katika magofu ya jengo la shule yao, kilichoharibiwa na kimbunga Freddy nchini Msumbiji.
© UNICEF
Watoto wakiwa wamesimama katika magofu ya jengo la shule yao, kilichoharibiwa na kimbunga Freddy nchini Msumbiji.

Watu 400,000 watawanywa na kimbunga Freddy Madagascar na Msumbiji: IOM

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Madagaska na Msumbiji imeongezeka huku makumi ya maelfu ya watu wakilazimika kuhama makwao baada ya kimbunga Freddy kupiga Madagaska tarehe 21 Februari na Msumbiji tarehe 24 Februari.  

Takriban watu 400,000 wanakadiriwa kuathirika katika nchi zote mbili kwani mvua kubwa, upepo mkali, mafuriko, na kuongezeka kwa viwango vya maji vimesababisha uharibifu mkubwa wa nyumba, shule, hospitali na miundombinu. 

IOM imekusanya rasilimali huku ikifanya kazi na serikali na jamii kuweza  kupunguza athari za kimbunga hicho kwa watu na maisha na imetoa msaada kwa makumi kwa maelfu ya watu katika vituo vya makazi ya muda kwenye nchi hizo mbili. 

Mtoto akitembea kupitia vifusi vya mijengo ya shule yao, iliyoharibiwa na kimbunga Freddy nchini Msumbiji.
© UNICEF
Mtoto akitembea kupitia vifusi vya mijengo ya shule yao, iliyoharibiwa na kimbunga Freddy nchini Msumbiji.

Nchini Msumbiji, IOM inaendelea kufuatilia na kutathmini athari za kimbunga hicho.  

Msaada unaotolewa na IOM 

Shirika hilo linafanya tathmini ya athari na mahitaji katika mikoa yote iliyoathiriwa kupitia mfumo wake wa ufuatiliaji wa watu kutawanywa (DTM) na kutoa usaidizi wa kiufundi na wa vifaa kwa serikali katika usimamizi wa vituo vya makazi vya muda. 

Pia shirika hilo linasaidia zaidi mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii, kuendesha mafunzo ya ulinzi dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kingono (PSEA) kwa wale wanaohusika katika kukabiliana na hali hiyo, pamoja na kuendeleza afya na usafi wakati nchi inakabiliwa na mlipuko wa kipindupindu unaoendelea.  

IOM imetuma vifaa 1,200 vya makazi ya dharura hadi Beira mwishoni mwa juma, ili kusambazwa kwa kaya zilizoathirika kwa uratibu wa taasisi ya kitaifa ya kukabiliana na majanga (INGD). 

Watu wakikimbia makazi yao wakati kimbunga Freddy kikizuka ardhini huko Vilanculos nchini Msumbiji.
© UNICEF
Watu wakikimbia makazi yao wakati kimbunga Freddy kikizuka ardhini huko Vilanculos nchini Msumbiji.

Waliopata hifadhi hadi sasa 

Kwa mujibu wa IOM hadi kufikia tarehe 01 Machi 2023, ripoti zinaonyesha jumla ya watu 12,744 wamepata hifadhi katika vituo 25 vya makazi ya muda huko Inhambane, Gaza na Sofala huku mahitaji ya dharura yakiwa ni makazi ya dharura, afya, ulinzi, chakula na maji, usafi wa mazingira na huduma za kujisafi (WASH). Takwimu hizi zinabadilika kwa kasi huku mvua zikiendelea kunyesha na vitongoji vikisalia na mafuriko. 

Nchini Madagaska, Shirika la IOM linafanya kazi kwa karibu na serikali na washirika wengine wa kibinadamu kusaidia karibu watu 80,000 walioathirika. IOM inasaidia usimamizi wa vituo na tathmini katika vituo 11 rasmi vya malazi ya muda huko Mananjary.  

Zaidi ya watu 37,000 wamelazimika kuyahama makazi yao huku zaidi ya nyumba 14,000 zikiathirika vibaya na mafuriko. 

Shirika hilo la uhamiji limesema kimbunga Freddy kimeongeza hali mbaya ya kibinadamu nchini Msumbiji, ambapo watu milioni 1 ni wakimbizi wa ndani kutokana na migogoro katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.  

Katika nchi zote mbili, mafuriko ya hivi karibuni yanaongeza zaidi hatari ya magonjwa kama vile kipindupindu na malaria, miongoni mwa mengine.