Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampuni Uganda zaitikia wito wa UN za hatua kwa tabianchi

Nchini Uganda, mwanamke mkazi wa Hoima akichambua plastiki kabla ya kurejelezwa.
UN/ John Kibego
Nchini Uganda, mwanamke mkazi wa Hoima akichambua plastiki kabla ya kurejelezwa.

Kampuni Uganda zaitikia wito wa UN za hatua kwa tabianchi

Tabianchi na mazingira

Nchini Uganda katika mji wa Hoima, kampuni moja imechukua hatua ya kutekeleza wito wa Umoja wa Mataifa wa kuchukua hatua kwa tabianchi kwa kuondokana na taka za plastiki zinazoharibu mazingira kwa kuzirejeleza katika njia ambayo siyo tu inasafisha mazingira bali pia inaleta kipato kwa waajiriwa wakiwemo wanawake na vijana.

Ni katika kitongoji cha Kyesiiga jijini Hoima ambapo nashuhudia wanawake wakichambua taka ya vyombo vya plastiki huku wnegine wakiipakia kwenye mashine ya kuisaga.

Mtambo huu ni wa kwanza kabisa katika eneo la magharibi ya kati mwa Uganda lenye miji mingi inayokua kwa kasi.

Ivan Semwogerere ni meneja wa mtambo huu ambao kwa sasa unaoshughulikia angalau tani 15 za taka ya plastiki kwa wiki. Bwana Ssemwogerere anasema, "Kabla ya kuvisagisha na kuviponda tunavileta hapa na kuvipima ili tujjue ni kilo ngapi tunazoingiza ndani hapa kwa siku. Kisha wanawake wanavichambua kulingana na rangi zake ili tufahamu ni kilo ngapi tuanzoingiza kwenye mashine. Baada ya kuvisagisha, tunavifunga na kuvipakia kwa ajili ya kusafirishwa hadi kiwandani Kampala."

Wataalamu wa mazingira wanasema plastiki kama hii inaweza kudumu kwa miaka zaidi ya 400 bila kuoza. Kampuni hii inasaidia sio tu kuokoa mazingira bali pia kutoa ajira kwa vijana. Meneja huyo wa mtambo anafafanua akisema, "Kuna wafanyakazi zaidi ya 50 kwa sababu kuna madereva, vijana wanaopakia na wanawake wanaochambua aina mbalimbali ya taka ya plastiki. Baadhi yao hawako tu hapa kwa sasa hivi kwani wamekwenda kufanya kazi kwingineko."

Huyu hapa ni mmoja wa wanufaika, "Jina langu ni Abiteekaniza Denis. Ni miaka miwili sasa tangu nije hapa kufanya kazi kwenye mashine hizi za kusagisha taka za plastiki. Imenisaidia sana kwa sababu nyumbani nimejenga nyumba na hata familia yangu inapata chakula bora. Nami najikimu kama vile mnavyoniona hapa"

Soundcloud

 

Vijana wa kike nao wamenufaika kama anavyoeleza Goret Nyamugo ambaye anasema, "Kwanza kabisa faida ninayopata ni kwamba ninapokea mshahara wa pesa zisizopungua shilingi laki moja. Kila wiki ninachambua taka hiyo ya plastiki inayoniingizia angalau shilingi 37,000, ikimaanisha mwisho wa mwezi ninapata zaidi ya shilingi laki tatu"

Meneja Semwogerere anasema usafirishaji ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili mathalani, "Katika njia moja ama nyingine tunasaidia kuokoa mazingira kwa sababu tani 60 za taka ya plastiki tunazoondoa katika mazingira kila mwezi zingeishia mitoni au ardhini. Nyingine zingeziba mifereji na kuingiza serikali kwneye gharama za kuzibua mifereji hiyo ya maji"

Anawaomba wadau mbalimbali kujiunga nao ili kuokoa mazingira akisema, "Kuna changamoto ya usafirishaji kwani taka ya plastiki huwa nyepesi lakini ni mzigo mkubwa. Unapata kwamba gunia moja la taka hiyo ina uzito wa kilo tano, mtu hatapata kilo tano apande pikipiki ya boda-boda inayohitaji shilingi elfu tano kufika hapa ilihali elfu tano hizohizo ndizo tutamlipa kuvinunua"

Kutoka hapa plastiki hii inasafirishwa hadi kwenye viwanda vya plastiki jijini Kampala kama malighafi na kisha kutumiwa kutengeneza upya vyombo vya plastiki.