Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iwe mvua iwe upepo mkali madarasa yetu ni salama: Mwanafunzi Msumbiji

Ujenzi wa madarasa nchini Mozambique yanayohimili hali mbaya za hewa ikiwemo vimbunga vinavyong’oa mapaa.
UN Habitat Mozambique
Ujenzi wa madarasa nchini Mozambique yanayohimili hali mbaya za hewa ikiwemo vimbunga vinavyong’oa mapaa.

Iwe mvua iwe upepo mkali madarasa yetu ni salama: Mwanafunzi Msumbiji

Tabianchi na mazingira

Kila mwaka, Msumbiji hukabiliwa na matukio ya hali mbaya za hewa kupindukia kama vile vimbunga na mafuriko, matukio ambayo husababisha uharibifu wa shule na hatimaye watoto kushindwa kujifunza. Hata hivyo, ujenzi wa madarasa yanayohimili matukio kama vile pepo kali na mafuriko umeleta nuru na matumiani kwa watoto, wazazi na walimu. Madarasa haya yanawezesha watoto kubakia salama hata wakati wa mvua na upepo mkali. Hali hii ni uwekezaji wa kudumu kwani ni  hakikisho kwa watoto kuendelea kupata elimu na mustakabali wao kuwa bora. 

Soundcloud

Mashariki mwa Msumbiji, kutoka angani, taswira mbili tofauti za mapaa ya shule ya msingi. Moja rangi ya buluu na nyingine mabati kuukuu. Moja kwa moja tunaingia darasani mwalimu anaandika ubaoni wanafunzi wananakili. Umsikiaye ni Catarina Magaia. Yeye ni mwanafunzi na anasema sasa shule yao ni nzuri na anapenda kujifunza.

Catarina ambaye hapa anasema ana umri wa miaka 10  na mwanafunzi shule ya msingi ya Changalane anakumbuka hali ilivyokuwa zamani.

“Zamani mvua iliponyesha hatukuweza kuketi darasani. Tuliweka madaftari yetu kwenye mifuko ya nailoni na kukimbilia nyumbani.”

Kwa watoto wengi kama Catarina nchini Msumbiji, fursa ya kuwa na mazingira bora ya elimu inazidi kuyoyoma kutokana na hali mbaya za hewa kupindukia.

Agostino Mobriga, Mkurugenzi wa shule ya msingi ya Josina Machel anaelezea, “Kulikuwa na maji mengi yanaingia darasani kiasi kwamba wanafunzi walilazimika kuondoka darasani.”

Ricardo Pondzole, Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya msingi Changalane naye anasema, “Hatukuona kuwa ni vema kwa wanafunzi wetu wahitimu masomo kwenye mazingira haya na baadaye wawe viongozi wa taifa hili.”

Kadri hatari kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi ilivyozidi kuongezeka, uwekezaji katika madarasa yaliyo salama na ya kuhimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi ukapatia wanafunzi fursa ya kuwa na maisha bora ya baadaye.

Hivyo Benki ya Dunia ikafadhili mradi wa kuimarisha madarasa kwa kukarabati au kujenga zaidi ya madarasa 700 nchini Msumbiji. Madarasa hayo yanaweza kuhimili dhoruba za upepo mkali na hata mafuriko. Gercia Mussanhane kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la makazi, UN-Habitat ambaye ni mhandisi wa Ujenzi anaelezea kilichofanyika, 

“Mradi huu ulijikita katika kuimarisha muundo wa paa ili kulipatia uimara na lising’oke. Hivyo tuliondoa paa la zamani na kuweka jipya. Kwa hiyo kwa muundo mpya, haiwezekani kabisa kwa paa kuvunjika na kuangukia watoto.”

Lakini mwaka 2023 kimbunga kikali Fredy kilipiga tena eneo hilo la mashariki mwa Msumbiji. Mtoto huyu aliyeko darasani akiwa na tabasamu anasema, Kimbunga Fredy kilipopiga, hakukuweko na dalili yoyote ya ufa kwenye shule yetu, wala uharibifu wowote.

Ukarabati na ujenzi wa madarasa ulijumuisha uwekaji wa makinga maji kwenye mapaa yaliyowezesha uvunaji wa maji ya mvua na hivyo kuepusha kutwama kwa maji shuleni. Felina Martin ni mzazi, anasema, “Hatujawahi kuwa na mazingira kama haya. Ninafurahi na jamii pia inafurahi.”

Catarina anatamatisha akisema, “Sasa mambo ni mazuri kwani tunaweza kusoma wakati wa baridi au wakati wa mvua.”