Ndoto yangu ni kurejea nyumbani na kuishi kwa amani : Islam Mubarak
Ndoto yangu ni kurejea nyumbani na kuishi kwa amani : Islam Mubarak
Kutana na Islam Mubarak msichana mwenye umri wa miaka 21 ambaye vita mpya iliyozuka Sudan Aprili mwaka jana ilimlazimisha kufungasha virago na familia yake na kuukimbia mji mkuu Khartoum na sasa amekwama katika kambi ya wakimbizi wa ndani katika jimbo la El-Gedarif, lakini ndoto yake ni kurejea nyumbani siku moja.
Katika kambi ya wakimbizi wa ndani inayosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ni Islam akiwa amekata tamaa kwa kutouona au kuelezea mustakbali wake.
Kabla ya kuzuka mapigano na kukimbia Khartoum Islam alikuwa akisomemea masuala ya fasihi ya Kiingereza, kisha maisha yake yakapinduliwa na ndoto yake kubadilika,
“Kama ungeniuliza hapo awali ningekueleza mustakbali wangu utakuwaje , ningemaliza masomo na kisha kwenda zangu Korea Kusini kukutana na kundi la muziki wa pop la BTS, lakini sasa siwezi kusema hivyo.”
Kama mmoja wa mashambiki wakubwa Islam anapata faraja kupitia muziki wa kundi maarufu la BTS na kwa kusoma taarifa zao.
“Niliingia kwenye Google nikarambaza na kusoma kuhusu maisha yao na ninaweza kulinganisha na maisha yangu kwa kiasi fulani, kwani walipitia changamoto kubwa kabla ya kuwa maarufu. Wanatoka Korea Kusini na walijisukuma sana kujifunza kuongea Kiingereza na hilo ndilo linaloniunganisha mimi na wao.”
Kwa mujibu wa UNHCR Islam ni miongoni mwa Wasudan zaidi ya milioni 7 waliofurushwa makwao hadi sasa na kulazimika kuwa wakimbizi ndani ya Sudan na katika nchi jirani na vita bado inaendelea. Islam anasema kambini maisha magumu,
“Hali hapa ni ngumu sana kwa wakimbizi wa ndani, ni vigumu kuielezea mtu anahitaji kuishi hapa na kuishuhudia , sijui cha kusema.”
Hata hivyo Islam ana matumaini kwamba vita itakwisha hivi karibuni ili akaendelee na masomo na kutimiza ndoto yake
“Maisha yetu Khartoum yalikuwa mazuri, nahisi mambo yatakuwa bora kwangu, hivyo hakuna shida kusubiri kidogo kabla ya kurejea Khartoum “
Na hilo ndilo UNHCR inalitaka kwa wakimbizo wote kutoka Sudan kama Islam.