Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sigrid Kaag wa Uholanzi ateuliwa Mratibu wa UN Gaza

Sigrid Kaag, Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi Mpya wa Gaza
UN /Evan Schneider
Sigrid Kaag, Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi Mpya wa Gaza

Sigrid Kaag wa Uholanzi ateuliwa Mratibu wa UN Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Sigrid Kaag kutoka Uholanzi ameteuliwa hii leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuwa Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza, ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2720 la mwaka huu wa 2023.

 

Azimio hilo lililopitishwa Ijumaa ya tarehe 22 mwezi huu wa Desemba, pamoja na mambo mengine lilimkataka Katibu Mkuu ateue Mratibu Mwandamizi ambaye atahusika na kuwezesha, kuratibu, kufuatilia na kuthibitisha kama ni sahihi shehena zinazotakiwa kuingia Gaza kwa usaidizi wa kibinadamu zinaingia.

Bi. Kaag atawajibika pia kuanzisha mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kuharakisha shehena kuingia Gaza kupitia nchi ambazo hazihusiki kwenye mzooz.

Katika kutekeleza majukumu yake, atashirikiana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi, (UNOPS).

Bi. Kaag anatarajiwa kuanza majukumu yake tarehe 8 mwezi Januari mwaka 2024.

Mratibu Mwandamizi huyu ana uzoefu wa kutosha kwenye masuala ya kisiasa, kibinadamu na maendeleo halikadhalika diplomasia.

Hivi karibuni alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Kwanza Mwanamke wa Fedha kwenye serikali ya Uholanzi tangu mwezi Januari mwaka 2022.

Ameshika nyadhifa mbali mbali serikalini ikiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na pia alifanikisha chama chake kushinda uchaguzi mwezi Machi mwaka 2021.

Ndani ya Umoja wa Mataifa, aliwahi kushika nyadhifa tofauti tofauti ikiwemo Mratibu Maalum wa UN nchini Lebanon kati ya 2015 na 2017 na pia Mratibu Maalum wa shirika la pamoja la kudhibiti silaha za kemikali na Ujumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria kuanzia 2013 hadi 2015.

Anazungumza Kiholanzi, Kijerumani, Kifaransa, Kiingereza, Kispanyola na Kiarabu.