Ushushaji misaada kutoka angani Gaza ni tone tu baharini - Sigrid Kaag
Ushushaji misaada kutoka angani Gaza ni tone tu baharini - Sigrid Kaag
Mratibu Mwandamizi wa masuala ya Kibinadamu na Ujenzi wa Gaza, Sigrid Kaag leo Machi 7 jioni ya saa za New York, Marekani amewadokeza wanahabari baadhi ya mambo aliyoyawasilisha leo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililofanya mashauriano ya faragha kuhusu hali ya Gaza.
"Ujumbe wangu kwa Baraza ulikuwa vilevile tunahitaji kujaza soko la Gaza na misaada ya kibinadamu, na vile vile kuwezesha tena sekta binafsi ili bidhaa za kibiashara ziweze kuingia ili kukidhi mahitaji ya raia." Amesema Kaag.
Kaag amesisitiza kwamba usaidizi wa kibinadamu "sio zoezi la kuhesabu malori na akaongeza, "Tunahitaji kujua ubora, umuhimu, tunahitaji kujua inakidhi mahitaji, na kama nilivyosema, kiasi.
Afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa Gaza pia amewaeleza waandishi wa habari kwamba amewafahamisha wajumbe wa Baraza la Usalama kuhusu umuhimu wa kubadilisha njia za usambazaji bidhaa kupitia ardhini.
Ameeleza kuwa utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa njia ya anga ni "ushuhuda kwa ubinadamu wetu wa pamoja, lakini ni tone baharini," akisisitiza kwamba kutumia ardhi "kunasalia kuwa suluhisho bora."
"Hili linasalia kuwa suluhisho bora. Ni rahisi, ni haraka, ni nafuu, hasa kama tunajua kwamba tunahitaji kuendeleza usaidizi wa kibinadamu kwa watu wa Gaza kwa kipindi kirefu.” Amesisitiza.
Pia ameeleza umuhimu wa kufungua vivuko vya ziada akisema, "msaada unapaswa kufika kupitia Ashdod lakini pia vivuko vingine, sio tu Kerem Shalom."
Kaag pia amesema, “Nimelitaarifu Baraza kuhusu mipango ya kina iliyoingia katika uundaji wa utaratibu chini ya azimio hilo, ambao kwa kweli unalenga kutoa uwazi, kuwezesha uhakiki wa ufuatiliaji, lakini pia kuongeza kasi ya misaada kufika Gaza.”
Ameendelea kusema, “Ni zoezi la kiufundi. Sitaelezea maelezo yote, lakini ni muhimu, kwa sababu kupitia utaratibu, tunaunga mkono familia ya kimataifa ya kibinadamu ili kupata misaada mahali inapohitaji kuwa ndani ya Gaza, bila kujali changamoto zote linapokuja suala la uwezo wa pamoja wa kufanya kazi katika hali zisizo na uhakika na zisizo salama, kutokana na matatizo yote ambayo wafadhili wa kibinadamu wamekabiliana nayo leo.
Alipoulizwa kuhusu mazungumzo ya azimio, Kaag amesema, "Nadhani lengo la wasuluhishi linabakia katika kujaribu kufikia makubaliano. Sote tunatumai, na Katibu Mkuu amesisitiza hili mara nyingi sana kwa ajili ya kuachiliwa kwa mateka. Ni muhimu kuwa na usitishaji vita.”
Lakini wakati huo huo, ameongeza, "jumuiya ya kibinadamu itafanya chochote iwezacho kukidhi mahitaji ya watu. Wana haki ya chakula. Wana haki ya makazi. Wanastahili kupata huduma ya afya, na wana haki ya kiwango cha ulinzi ambacho mtu angetarajia licha ya hali ngumu sana.