Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande zinazozozana mashariki mwa DRC zakumbushwa wajibu wa kulinda raia

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na wa Misaada ya Kibinadamu Bruno Lemarquis alipozuru DRCongo mapema Machi
© UNOCHA
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na wa Misaada ya Kibinadamu Bruno Lemarquis alipozuru DRCongo mapema Machi

Pande zinazozozana mashariki mwa DRC zakumbushwa wajibu wa kulinda raia

Amani na Usalama

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Bruno Lemarquis, ameonesha wasiwasi mkubwa kuhusu ghasia zinazoongezeka katika mji wa Mweso, ulioko takribani kilomita 100 kutoka Goma, katika jimbo la Kivu Kaskazini (mashariki mwa DRC), Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaeleza Waandishi wa habari jijini, New York Marekani.

Katika taarifa iliyoambazwa leo, Bwana Lemarquis amesema kuwa kutokana na makumi ya raia kuuawa, jumuiya ya kibinadamu nchini humo inasikitishwa na ukiukwaji mkubwa unaofanywa huko ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.

“Amezikumbusha pande zinazozozana wajibu wao wa kulinda raia, kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa kibinadamu na kuhakikisha kwamba msaada unaweza kuwafikia wale wanaohitaji zaidi.” Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amewaeleza Waandishi wa habari ambao wametaka kujua masuala mbalimbali yanayoendelea katika ulimwengu wa Umoja wa Mataifa likiwemo hili la DRC.

Dujarric amefafanua zaidi taarifa kutoka DRC kwamba athari za kibinadamu kutokana na kuongezeka kwa vurugu hivi karibuni zimekuwa za kutisha. Wanaume, wanawake na watoto wapatao 8,000 wamekimbia makazi yao na kutafuta makazi karibu na Hospitali ya Mweso. “Kwa ujumla, zaidi ya robo milioni ya watu (watu 250,000)  katika eneo la afya la Mweso wanahitaji msaada wa kibinadamu haraka.”