Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya watu wakimbia ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Makazi ya Wakimbizi wa ndani, IDP huko Sake, Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire
Makazi ya Wakimbizi wa ndani, IDP huko Sake, Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Maelfu ya watu wakimbia ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Amani na Usalama

Kufuatia hali ya ghasia zilizinazozidi kuongezeka kati ya vikosi vya serikali na makundi yasiyo ya kiserikali yenye kujihami kwa silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, lina wasiwasi mkubwa kuhusu yanayoweza kuwakuta wananchi.

Kutoka katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Goma, unaisikia milio ya makombora na hata unaweza kuona mwanga wa makombora hayo yakipita angani umbali mfupi tu kutoka katika kambi hii ambayo vijumba na maturubai meupe yenye nembo ya UNHCR angalau kuwasitiri wakimbizi hawa dhidi ya mvua yametapakaa na msongamano wake ni wa kutisha. Huyu amebeba mtoto, yule amebeba dumu na maji, na mwingine godoro hali ambayo inaonesha kila mtu ameishikilia roho yake mkononi.

Lazaro, ni mmoja wa mmoja wa wakimbizi wa ndani aliyekimbia na watoto wake anasema, “Nilikimbia kutoka Mushake hadi Sake. Baada ya miezi mitatu, hali ilizidi kuwa mbaya tena, nilitoroka kurudi hapa Goma jana.”

UNHCR na wadau wake wamesitushwa kutokana na ripoti za mabomu kuanguka kwenye maeneo ya kiraia, ikiwa ni pamoja na eneo la Zaina huko Sake na eneo la Lushagala huko Goma, ambapo wakimbizi wa ndani zaidi ya 65,000 wanaishi, jambo linalozua wasiwasi mkubwa juu ya usalama wao.

Hayo yanayosemwa na UNHCR, Lazaro ameyashuhudia kwa macho yake, “Njiani tulikumbana na hali ngumu kadhaa, ikiwemo mashambulizi ya mabomu. Tulipoteza kila kitu, kwa sababu tulikimbia ghafla wakati mabomu yalianza kulia, na tukakimbia hadi hapa.

Uwepo wa vilipuzi ambavyo havijalipuka bado kunasababisha tishio fulani kwa watoto. Tangu wiki ya kwanza ya Februari, takriban raia 15 wameuawa na 29 kujeruhiwa karibu na Goma na Sake. Mashambulio hayo ya kiholela ya mabomu yanazidisha matatizo katika rasilimali ambazo tayari ni chache ili kuwahudumia wakimbizi wa ndani 800,000 katika eneo hilo, na wengine milioni 2.5 waliokimbia makazi yao katika Mkoa wa Kivu Kaskazini.

Vurugu zinaendelea kuzuia ufikiaji wa watu waliotengwa katika eneo la Masisi na Rutshuru, na kuongeza changamoto zinazokabili mashirika ya kibinadamu katika kutoa msaada muhimu. Kukiwa na machaguo machache yananazowezekana kwa sasa ya kupita kwa usalama kutoka Goma, jamii zilizofurushwa zinazoongezeka zilizohamishwa katika mji zinakabiliwa na hali mbaya inayoongezeka haraka.