Baraza la Usalama toa kauli kuhusu MONUSCO kuondoka DRC
Baraza la Usalama toa kauli kuhusu MONUSCO kuondoka DRC
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litoe kauli yake kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na Pili mwezi Agosti mwaka huu kwenye ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuondoka kwa ujumbe wa Umoja huo wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO.
Kauli hiyo ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bintou Keita na Mkuu wa MONUSCO ameitoa leo akihutubia Baraza hilo jijini New York, Marekani lililokutana kujadili hali ya usalama kwenye taifa hilo la Maziwa Makuu ambako vita mashariki mwa nchi hiyo imesababisha janga la kibinadamu.
Ripoti hiyo ya Katibu Mkuu ilipendekeza pamoja na na mambo mengine mbinu nyingine za muundo wa MONUSCO na mustakabali wa miundo mingine ya Umoja wa Mataifa nchini huo zaidi ya majukumu ya sasa ya ujumbe huo.
DRC imepitisha mpango wa MONUSCO kuondoka kasi
Bi. Keita amesema tayari mamlaka za DRC zimepitisha mpango uliorekebishwa wa kuondoka kwa MONUSCO nchini humo akisema, “hii ni hatua muhimu kuelekea kuongeza kazi ya kuondoka kwa ujumbe huo, huku ukihakikisha mchakaot huo unatekelezwa taratibu lakini kiuwajibikaji.”
Amesisitiza kuwa MONUSCO hivi sasa itashirikiana na mamlaka za DRC kuelekea utekelezaji wa mpango huo, huku ikiendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Baraza la Usalama.
Hata hivyo amesema cha kusikitisha MONUSCO inaendelea kulengwa na taarifa potofu na za uongo, pamoja na vitisho vya kushambuliwa huku akishutumu mauaji ya raia yaliyofanywa na vikosi vya taifa vya usalama tarehe 30 mwezi uliopita wa Agosti na kwenye mji wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini.
MONUSCO iondoke ili tuondoe mvutano wake na raia- DRC
Serikali ya DRC ilipata fursa ya kuzungumza kwenye Baraza hilo kupitia Naibu Waziri wake Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Christophe Lutundula.
Yeye amesema mpango wa marekebisho ulioandaliwa kimkakati na serikali ya DRC kuhusu kuondoka kwa MONUSCO unalenga; kuondoa mvutano uongezekao kila uchao kati ya MONUSCO na raia, kuepuka kujirudia kwa matukio ya majonzi yatokanayo na shinikizo la kuondoka kwa vikosi vya UN au kuondoka kwa ghasia.”
Bwana Lutundula amesema, “kipaumbele chetu kikuu ni kurejesha amani na usalama nchini kote. Na hii ni fursa ya kusisitiza kuwa ni wakati kwa Umoja wa Mataifa (UN) na hasa Baraza la Usalama lijifunze kutokana na mipango yake ya kuingilia masuala ya aAfrika na kubadilisha mfumo wake wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye bara letu.”
Nitazungumza na Bwana Lutandala
Waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri nje ya ukumbi kuzungumza na Bi. Keita walipata fursa hiyo ambapo Mkuu huyo wa MONUSCO aliwaeleza kuwa atakutana na Bwana Lutundula kujadili kile kilichopendekezwa katika ngazi ya kiufundi, ambacho kimsingi ni kufahamu masharti..
“Nisemapo masharti, ni kwamba ni mambo yapi yanapaswa kutekelezwa kwa ajili ya kuondoka na kwa njia wajibifu na kusonga mbele kwa MONUSCO.”
Akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Rais wa DRC Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo alieleza kuwa tayari wametuma barua kwa Baraza la Usalama ili kusongesha kasi ya kuondoka kwa MONUSCO nchini humo kuanzia Desemba mwaka huu wa 2023 badala ya Desemba 2024.
![]() | DRC uchaguzi mkuu kufanyika mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyopangwa Uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC utafanyika kama ilivyopangwa mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 na wakati huo huo tunaomba kutekelezwa kwa ombi letu la kuongeza kasi ya kuondoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. news.un.org |
