Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ECOSOC wajadili kuhusu mustakabali wa ajira duniani

Balozi Paula Narvaez Ojeda wa Chile, Rais wa Kikao cha 2024 cha Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC).
UN Photo/Mark Garten
Balozi Paula Narvaez Ojeda wa Chile, Rais wa Kikao cha 2024 cha Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC).

ECOSOC wajadili kuhusu mustakabali wa ajira duniani

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC hii leo huko Santiago, Chile wamefanya mkutano wa kujadili kuhusu mabadiliko ya kasi katika ulimwengu wa kazi na upi mustakabali wake. 

ECOSOC wamejadili hayo kwa kuzingatia ukweli kuwa ingawa masuala kama teknolojia mpya zinazoibukia kila siku, utandawazi, na mielekeo ya idadi ya watu hutoa fursa za kusisimua za uboreshaji wa tija na uvumbuzi, lakini ukweli ni kuwa fursa hizo zinakuja na changamoto kwa wafanyakazi na watunga sera.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais wa ECOSOC Paula Narváez amesisitiza jinsi kazi zenye heshima, utebngenezaji wa nafasi za kazi, ulinzi wa kijamii, haki za wafanyakazi, na mazungumzo ya kijamii ni muhimu kwa maendeleo endelevu.

Bi Narváez ametoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji ili kuunda kazi zenye staha zaidi.

“Ushirikiano mkubwa, ufadhili wa ziada wa kimataifa, na usaidizi wa kiufundi unaweza kukamilisha rasilimali za kitaifa ili kupanua kazi nzuri na ufikiaji wa ulinzi wa kijamii. Juhudi zilizoratibiwa zinahitajika ili kukabiliana na kutokuwepo kwa sera pamoja na kutunga sera zinazohitajika za kusaidia uwepo wa mishahara itakayo wawezesha watu kuishi, kandarasi salama na mazingira mazuri ya kazi,” alisema Rais huyo wa ECOSOC.

Kuhakikisha fursa za baadaye

Katika ujumbe wake alioutoa kwa njia ya video Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed ameonya kuwa “sindano haitasonga katika mwelekeo wa matarajio yetu” isipokuwa pale tu nchi zitakapo tii ahadi za kutomwacha mtu nyuma.

“Hii ina maanisha kukabiliana na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira kwa vijana, tofauti za kijinsia zinazoendelea katika eneo la mishahara, ushiriki wa soko la ajira na upatikanaji wa hifadhi ya jamii,” alisema Bi. Mohammed.

Aliongeza kuwa “maboresho ya kidijitali bila udhibiti” pia ni kichocheo cha ukosefu wa usawa.

“Zinapotumiwa ipasavyo, zana za kidijitali zinaweza kuharakisha uundaji wa kazi na kusaidia kupanua ulinzi wa kijamii, kama inavyoonekana katika nchi nyingi wakati wa coronavirus">COVID-19 - wakati ambapo pia tuligundua thamani ya kukuza jamii zinazojali.”