Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa ILO Houngbo afanya ziara ya kwanza nchini Senegal

Wanawake wa vijijini wakiuza jam ya kupaka mkate inatotengenezwa na maembe na viazi vitamu katika duka la kusindika chakula huko Bantantinnting, Senegal.
UN Photo/Evan Schneider
Wanawake wa vijijini wakiuza jam ya kupaka mkate inatotengenezwa na maembe na viazi vitamu katika duka la kusindika chakula huko Bantantinnting, Senegal.

Mkuu wa ILO Houngbo afanya ziara ya kwanza nchini Senegal

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO Gilbert F. Houngbo yuko ziarani nchini Senegal, ikiwa ni ziara yake ya kwanza kufanywa na kiongozi wa shirika hilo nchini humo. 

Bwanda Houngbo anatumia fursa ya ziara yake hiyo ya siku 4 kujadili na mamlaka na vyama vya wafanyakazi mwelekeo wa ajira katika dunia ya sasa hususan ajira yenye hadhi kwa vijana na wanawake, ulinzi wa wafanyakazi wahamiaji na urasimishaji wa uchumi usio rasmi.  

Kattika ziara hiyo itakayokamilika Januari 25 atakutana na kujadiliana na Rais wa Senegel Macky Sall, jumuiya za wafanyakazi nchini humo na kuwasilisha mradi wake wa “Muungano wa kimataifa kwa ajili ya haki ya kijamii” 

 Wengine atakaokutana nao ni mawqziri wa kazi, ajira na mafunzo ya ufundi stadi, lakini pia sekta za Kazi za mikono na Sekta Isiyo Rasmi.  

Pia atakutana na washirika wa kijamii  ambao ni mashirika ya waajiri na Wafanyakazi na mfumo wa Umoja wa Mataifa au "Timu yaUmoja wa Mataifa nchini humo". 

Masuala yatakayopewa uzito 

Masuala yatakayojadiliwa katika ziara yake ni pamoja na ajira zenye staha, hasa kwa vijana na wanawake, uhamiaji wa kazi na ulinzi wa wafanyakazi wahamiaji, upanuzi wa hifadhi ya kijamii, kurasimisha uchumi usio rasmi, migogoro na mazungumzo ya kijamii, na heshima ya viwango vya kimataifa vya kazi. 

Houngbo pia anatarajiwa kuzungumza kuhusu “Muungano wa Kimataifa wa Haki ya Kijamii, mpango wa kukuza kipaumbele cha haki ya kijamii na kupunguza usawa katika uundaji wa sera za kitaifa na kimataifa, na pia katika ushirikiano wa maendeleo, mikataba ya kifedha, biashara na uwekezaji.” 

Atafanya ziara zingine za ndani ya nchi 

Mkurugenzi huyo mkuu wa ILO pia amepanga kutembelea kijiji cha sanaa cha Soumbédioune, kwenye pwani ya magharibi ya Dakar, ambapo atakukutana na mafundi wa sanaa ambao ni wanufaika wa mradi wa ILO na Ubelgiji unaofanya kazi ya kujenga mifumo thabiti ya kitaifa ya ulinzi wa kijamii ili kuwashughulikia wafanyikazi katika sekta ya uchumi usio rasmi na familia zao, kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya na kuwawezesha watu hao kukabiliana na changamoto za kesho nchini Senegal. 

Bwana Houngbo  amerwakaribisha waandishi wa habari kufuatilia shughuli mbalimbali za ziara hii na atafanya mkutano nao mwishoni mwa ziara yake siku ya Ijumaa tarehe 27 Januari mjini Dakar.