Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Masaibu ya kutakiwa kuhama kila uchao yanaendelea Gaza

Mvulana mdogo anatazama nje ya hema katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Khan Younis anakoishi sasa. (Maktaba)
© UNICEF/Eyad El Baba
Mvulana mdogo anatazama nje ya hema katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Khan Younis anakoishi sasa. (Maktaba)

Masaibu ya kutakiwa kuhama kila uchao yanaendelea Gaza

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo linaendelea na siku ya pili ya mkutano wake wa kutafuta namna ya kumaliza mzozo mbaya unaoendelea huko Gaza huku kukiwa na kuongezeka kwa mvutano huko Mashariki ya Kati. 

Wasaidizi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wameendelea kueleza wasiwasi wao mkubwa kwa Wapalestina walio hatarini ambao kwa mara nyingine tena wanalazimika kukimbia vita kutokana na kuendelea kutolewa kwa amri za kutakiwa kuondoka maeneo waliyoko na kwenda kusaka hifadhi sehemu nyingine. 

Akirejelea wasiwasi huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya katika ukurasa wake wa X kwamba pamoja na tishio la kuuawa, watu wa Gaza wanakabiliwa na hatari ya magonjwa, wakati huu ambapo huduma za afya zinazidi kuporomoka.

Ni hospitali 16 tu kati ya 36 “zinazofanya kazi kwa kiasi fulani”, Alisema Katibu Mkuu Guterres.

Katika chapisho lingine kwenye mtandao wa kijamii, Mkuu wa Umoja wa Mataifa anyehusika na masuala ya misaada ya dharura Martin Griffiths amesema kwamba “hakujawa na utulivu katika ukatili unaofanywa huko Gaza tangu Oktoba 7 wakati mashambulizi ya Israel yalipoanza kujibu mashambulizi ya Hamas nchini Israel ambayo yaliacha 1,200 wakipoteza maisha na takriban 250 kuchukuliwa mateka. 

Zaidi ya Wapalestina 25,000 wameripotiwa kuuawa “ikiwa ni pamoja na akina mama wawili kila saa”, Bw. Griffiths alisema, akinukuu takwimu kutoka kwa mamlaka ya afya ya Gaza, huku hospitali zikiendelea “kuzidiwa, kuzingirwa na kuchomwa moto; nyumba zimeharibiwa na kuwa vifusi…maeneo ya usalama yamekuwa sehemu za hatari”.

Maisha ya tabu

Huku taarifa za “watu wengi kuhama makazi yao” zikiendelea kuripotiwa wakielekea kusini kutokea eneo la Khan Younis ambapo mapigano makali yanaendelea tangu mwanzoni mwa wiki, shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema waliowasili sasa wameweka mahema makubwa ya plastiki kwenye uzio wa mpaka unaotenganisha Rafah, kusini mwa Gaza kutoka katika nchi ya Misri.

Katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya OCHA imesema kuwa mapigano yanayoongezeka katika eneo la Khan Younis siku ya Jumatatu yamesababisha vifo vya watu kadhaa.

“Hali kwa ujumla inazidi kuzorota kwa kiasi kikubwa,” alisema msemaji wa UNRWA Adnan Abu Hasna. 

Hasna amebainisha kuwa mji wa Rafah sasa ni makazi ya watu milioni 1.3 na “hauwezi kabisa kustahimili” wimbi kama hilo, lililoshuhudiwa huko Rafah siku ya Jumanne na maafisa wakuu Sigrid Kaag, Mratibu Mwandamizi wa Misaada ya Kibinadamu na Ujenzi wa UN huko Gaza, na Jamie McGoldrick, Mratibu wa muda wa Misaada ya Kibinadamu kwa Eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.

Tishio la magonjwa 

Magonjwa kama vile homa ya uti wa mgongo na hepatitis C yanaenea pamoja na kuongezeka maradufu kwa idadi ya watu walio na magonjwa ya matumbo na ngozi ambayo yanatishia kusukuma huduma za afya kufikia hatua mbaya,

Bwana Hasna ameeleza kuwa misaada zaidi ya kibinadamu inahitajika kuingia Ukanda huo. ambapo “kila mtu yuko hatarini…iwe katika eneo la Khan Younis au Rafah.

“Hakuna mahali salama kabisa, lakini tunafikiri kuwa kuwasukuma wakazi zaidi wa Palestina kwenye mji wa Rafah ni kusukuma mambo kuelekea kwenye mlipuko.”

Elimu imesimama

Katika ukurasa wa et kwenye X siku ya Jumatano – 

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Elimu shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO limeripoti kwamba shule zake zote huko Gaza bado zimefungwa na nyingi kumegeuka kuwa nyumbani kwa Wapalestina zaidi ya milioni 1.2, kwa ujumla waliokimbia makazi yao.

Takriban wakimbizi wa ndani 340 sasa wameuawa walipokuwa wakitafuta usalama katika makazi ya UNRWA huku zaidi ya 1,100 wakijeruhiwa, limesema shirika hilo.

Majengo matatu kati ya manne ya shule katika Ukanda huu pia yamepata uharibifu pamoja na taasisi nyingi za elimu ya juu. 

UNWRA imebainisha kuwa mashambulizi kwenye vituo vya elimu na majengo ya Umoja wa Mataifa “yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu”. Tangu kuanza kwa vita, zaidi ya wanafunzi 625,000 na walimu 22,564 katika eneo hilo “wamenyimwa elimu na mahali salama kwa zaidi ya miezi mitatu.”

Na huku milio ya roketi ikiendelea kuripotiwa kutoka Gaza hadi Israel, shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilibainisha kuwa “maelfu ya wanafunzi na wafanyakazi wa elimu” walikuwa miongoni mwa waliouawa.

Nako huko katika Ukingo wa Magharibi, “kuongezeka kwa ghasia” pia kumetatiza upatikanaji wa masomo, UNRWA ilisema, kabla ya kurudia wito wake wa kukomesha mzozo huo.