Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madaktari Gaza wamejawa hofu kutokana na mlipuko wa magonjwa huku timu za misaada zikikimbizana kutoa huduma

Madaktari wa upasuaji wa wakimfanyia upasuaji mgonjwa katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza. (Maktaba)
WHO
Madaktari wa upasuaji wa wakimfanyia upasuaji mgonjwa katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza. (Maktaba)

Madaktari Gaza wamejawa hofu kutokana na mlipuko wa magonjwa huku timu za misaada zikikimbizana kutoa huduma

Amani na Usalama

Wakati usitishaji wa mapigano huko Gaza ukionekana kuingia siku ya tano leo, wahudumu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wameonya kwamba uwasilishaji wa misaada unahitajika kuongezeka haraka ili kuokoa maisha ya waliojeruhiwa na kujaribu kuzuia hatari ya mlipuko mbaya wa magonjwa ambao umewaacha madaktari wakiwa na hofu kubwa.

Vipaumbele muhimu ni pamoja na kusafirisha mafuta hadi kaskazini mwa eneo lililoathiriwa na vita, ili yatumike kuimarisha uwezo wa hospitali, kutoa huduma ya maji safi na kudumisha miundombinu mingine muhimu ya kiraia.

Huduma kama hizo zimeathiriwa sana na majuma kadhaa ya mashambulizi ya Israel kujibu mauaji ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba kusini mwa Israel ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200 na karibu watu 240 kuchukuliwa mateka. Mamlaka za afya za Gaza zimeripoti kuwa zaidi ya watu 15,000 wameuawa katika mashambulizi hayo hadi sasa.

Mtoto akilia baada ya kufiwa na mwanafamilia katika hospitali ya Nasser Medical iliyoko Khan Younis.
© UNICEF/Abed Zaqout
Mtoto akilia baada ya kufiwa na mwanafamilia katika hospitali ya Nasser Medical iliyoko Khan Younis.

Tishio kutoka angani na ardhini

Katika taarifa kutoka kusini mwa Gaza, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, James Elder amesema kuwa daktari kutoka hospitali ya Al-Shifa kaskazini alimwambia kwamba tishio kwa watoto "limetoka angani na sasa liko ardhini", aina ya kuhara na maambukizi ya magonjwa ya kupumua.

"Alikuwa na hofu kama mtaalamu wa matibabu katika suala la mlipuko wa ugonjwa ambao unanyemelea hapa na jinsi ambavyo utaathiri watoto ambao kinga zao na ukosefu wa chakula ... unawafanya kuwa dhaifu sana," ameongeza Bwana Elder.

Wakati mazungumzo yakiendelea ili kuachiliwa kwa mateka zaidi na ili kurefusha muda wa kusitisha mapigano, UNICEF imezungumza juu ya kusikitishwa kwake kuona vijana wengi wakihaha kunusuru maisha yao, "wakiwa na majeraha ya kutisha ya vita, wamelazwa na wengi wakilala kwenye maegesho ya magari kwa muda katika magodoro, wengine kwenye bustani kila mahali, madaktari wakilazimika kufanya maamuzi ya kutisha juu ya nani wanampa kipaumbele”.

Vifaa vya afya vinatayarishwa kwa usafirishaji hadi Gaza. (Maktaba)
© WHO
Vifaa vya afya vinatayarishwa kwa usafirishaji hadi Gaza. (Maktaba)

Ucheleweshaji mbaya

Mvulana mwingine ambaye mguu wake ulilipuliwa katika mashambulizi hayo alikuwa ametumia “siku tatu au nne akijaribu kufika Kusini mwa Gaza, akicheleweshwa na vituo vya ukaguzi,” amesema Bwana Elder akiendelea kuwa "Harufu ya kuoza ilikuwa wazi na mvulana huyo alikuwa amevunjika vipande vipande kila mahali. Yawezekana, alikuwa kipofu na alikuwa na majeraha ya moto hadi asilimia 50 ya mwili wake.”

Likielezea wasiwasi mkubwa juu ya ukubwa wa mahitaji huko Gaza, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO limebainisha kuwa tathmini iliyofanywa kaskazini mwa mwanzo wa kusitishwa kwa mapigano tarehe 24 Novemba imeonyesha kuwa "kila mtu kila mahali ana mahitaji makubwa ya afya" .

Akizungumza mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa WHO Dkt. Margaret Harris amesema kuwa hii ni "kwa sababu wana njaa, kwa sababu wanakosa maji safi na wamerundikana pamoja. kimsingi, ikiwa wewe ni mgonjwa, ikiwa mtoto wako ana hara, kama una maambukizo ya kupumua, hutapata msaada wowote.”

Katika taarifa yake ya hivi karibuni kabisa, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, ilisema kuwa uwasilishaji wa vifaa vya msaada umeharakishwa kusini mwa Wadi Gaza, ambapo kiasi kikubwa cha wakimbizi wa ndani milioni 1.7 wamesaka hifadhi. 

"Watoa huduma wakuu, ikiwa ni pamoja na hospitali, maji na vifaa vya vyoo na makazi, wameendelea kupokea mafuta kila siku kuendesha jenereta, imesema OCHA.