Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan: Kulengwa kwa makabila na makundi madogo kwashamirisha kauli za chuki - Mtaalamu wa UN

Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah nchini Sudan  kufuatia mapigano ya hivi karibuni.
© UNICEF/UNI492302/Mohamdeen
Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah nchini Sudan kufuatia mapigano ya hivi karibuni.

Sudan: Kulengwa kwa makabila na makundi madogo kwashamirisha kauli za chuki - Mtaalamu wa UN

Haki za binadamu

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Sudan, Radhouane Nouicer amesema kwa sasa nchini humo baadhi ya makundi yanalenga watu wa makabila u makundi madogo kitendo ambacho kinashamirisha kauli za chuki.

Bwana Nouicer amesema hayo akihojiwa kwa njia ya simu na Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa huku akisema kitendo hicho ni miongoni mwa matukio ya ukiukwaji mkubwa wa haki za msingi za binadamu kwenye taifa hilo ambalo mzozo wake unakaribia kutimu miezi 10 tangu uanze mwaka jana mwezi Aprili.

Mtaalamu huyo amesema kitendo hicho cha makundi mengine kushambulia makabila madogo “kinachochea kauli za chuki katika maeneo mengi ya nchi. Sasa imetosha.”

Kuteswa, vipigo vyashamiri

Ameongeza kuwa “tumeshuhudia watu kuuawa kiholela, mashambulizi kwenye maeneo binafsi na ya kiraia, watu kuswekwa korokoroni kinyume cha sheria wakiwemo wanaharakati wa haki za binadamu na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.”

Vitendo vingine ni watu kuteswa, vipigo, uporaji wa mali za umma na za watu binafsi, na vile vile kupatikana kwa makaburi walimozikwa watu wengi.

Ukatili wa kingono na wa kijinsia umeshamiri huku uchumi nao ukiporomoka akisema, “kwa sasa asilimia 46 ya wasudan hawana ajira. Thamani ya sarafu ya Sudan imeporomoka na mfumuko wa bei kwa miezi michache iliyopita umefikia asilimia 250.”

Giza limetanda pia kwa watoto wa Sudan kwani milioni 19 hawako shuleni.

Pamoja na ukimbizi, watu kushindwa kushiriki kwenye shughuli za kilimo kwenye taifa hilo lenye ardhi ya rutuba.

Ukwepaji sheria matokeo ya kinachoendelea sasa

Alipoulizwa kuhusu wito wake wa kutaka kuona vitendo vyote vya ukiukwaji wa haki na sheria za kimataifa za haki za binadamu vinachunguzwa nah atua kuchukuliwa haraka mtaalamu huyo amesema kwa mtazamo wake miongo kadhaa ya ukiukwaji wa haki Sudan ndio chanzo cha manyanyaso na ukatili wote unaoshuhudiwa hivi sasa nchini humo.

“Licha ya kwamba maazimio mengi yamepitishwa na pande kinzani, pamoja na kuanzishwa kwa mifumo na kamati za kupitia vitendo hivyo vya ukiukwaji wa haki au madai ya ukiukwaji wa haki, hakuna chochote kimefanyika,” ametanabaisha mtaalamu huyo.

Hivyo amesema anadhani kipaumbele kwa Sudan sasa ni kukomesha ukwepaji sheria na kuwafikisha mbele ya sheria watekelezaji wa vitendo hivyo,” amesema Bwana Nouicer.