Ghasia zikiendelea Sudan, chonde chonde watoto walindwe- UNICEF

23 Januari 2019

Kufuatia ripoti ya kwamba watoto ni miongoni mwa watu waliouawa kwenye ghasia nchini Sudan, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesihi mamlaka nchini humo kuhakikisha watoto wanalindwa na haki zao za msingi zinazingatiwa.

UNICEF katika taarifa iliyotolewa leo mjini Amman, Jordan inasema kuwa yaripotiwa watoto waliuawa, wengine kujeruhiwa kwenye ghasia hizo zinazoendelea za kupinga ongezeko la bei za bidhaa na ugumu wa maisha nchini humo huku watoto wengine wangali wanashikiliwa korokoroni.

Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Geert Cappelaere amesema ingawa bado ni vigumu kwa shirika hilo kuthibitisha ripoti hizo, watoto wanapaswa kulindwa wakati wote dhidi ya aina yoyote ya ghasia, ukatili na kutendewa hovyo iwe kimwili au kiakili.

Amesema watoto katu hawapaswi  kulengwa wala kutumikishwa.

UNICEF inasema kuwa katika miezi ya hivi karibuni, Sudan imeshuhudia ongezeko la aina yake la gharama za maisha na  uhaba wa mkate na mafuta, huku umaskini miongoni mwa watoto na kaya zao ukiongezeka na hivyo kulazimu kaya kuchukua hatua zisio na maslahi kwa watoto kama vile kuwaondoa watoto wao shuleni.

Hali hiyo ya uhaba wa bidhaa, kwa mujibu wa UNICEF  imesababisha watoto wengi nchini Sudan kuhitaij huduma ya afya na lishe.

Kwa mantiki hiyo, Bwana Cappelaere ametoa wito kwa mamlaka nchini Sudan kupatia kipaumbele ulinzi wa watoto na haki zao za elimu na afya kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter