Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tahadhari za mapema kuhusu maji na majanga ni muhimu:WMO

Majanga yatokanayo mafuriko yanababisha usumbufu, majeruhi wengi na hasara kubwa za kiuchumi katika sehemu mbalimbali za dunia.
Dinga Bienvenue/Congo National Hydrological Service
Majanga yatokanayo mafuriko yanababisha usumbufu, majeruhi wengi na hasara kubwa za kiuchumi katika sehemu mbalimbali za dunia.

Tahadhari za mapema kuhusu maji na majanga ni muhimu:WMO

Tabianchi na mazingira

Kikosi cha wataalamu kuhusu huduma za tahadhari ya mapema kimekutana katika Shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya Hewa Duniani, WMO huko jijini Geneva, Uswisi, kutathimini hali ya  Jamhuri ya Congo Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na nchini Mauritius, ili kuendeleza mpango wa kimataifa wa kutoa tahadhari za mapema kwa wote na pia kuchukua hatua kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji na kupunguza hatari zinazohusiana na maji. 

Haja ya kuchukua hatua za pamoja ilisisitizwa tena na mfululizo wa majanga ya mafuriko ambayo yamesababisha usumbufu na hasara nyingi za kiuchumi katika sehemu mbalimbali za dunia.

Wataalam hao wamesema Idadi kubwa ya majanga yanahusiana na maji na kwa hivyo usimamizi na ufuatiliaji wa maji ndio kiini cha msukumo ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuhakikisha kwamba kila mtu amefikiwa na mifumo ya tahadhari za mapema dhidi ya majanga kufikia mwisho wa mwaka wa 2027.

Kwa mujibu wa wataalam hao nyingi kati ya nchi 30 zilizolengwa kuchukuliwa hatua za kipaumbele katika tahadhari ya mapema kwa wote  zilikumbwa na mafuriko makubwa au ukame mwaka wa 2022. 

Hakuna hata nchi moja iliyokuwa na takwimu za kihaidrolojia kwa wakati na sahihi ili kusaidia kufanya maamuzi kulingana na ushahidi na hatua za mapema, kulingana na ripoti ya WMO kuhusu rasilimali za maji duniani. 

Mauritius ambayo ni moja ya nchi 30 zilizolengwa ilikumbwa na mafuriko makubwa yanayohusiana na kimbunga tarehe 15 Januari mwaka huu.

Kuhusu Jamhuri ya Congo, wataalam hao wamesema Bonde la Congo linakabiliwa na mafuriko makubwa zaidi hivi sasa katika kipindi cha takriban miongo sita .

Wataalam hao wamesema mvua kubwa iliyonyesha tangu Oktoba mwaka jana, 2023 ilipasua kingo karibu na Mto Ubangi, mojawapo ya mito mitatu mikuu inayotiririka katika Bonde la Congo. 

Dharura ya mafuriko ilitangazwa rasmi na serikali tarehe 29 Desemba. Ofisi ya kratibu masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema tangu tarehe 19 Januari zaidi ya watu 350,000 wanahitaji msaada wa kibinadamu nchini Congo, ambapo idara tisa kati ya 12 za nchi hiyo zimesalia chini ya maji. 

Vijiji vingi vinaweza tu kufikiwa kwa mashua au mitumbwi na maeneo makubwa ya ardhi yenye tija ya kilimo yamefurika. 

Hali ni mbaya pia DRC

Dkt. Jean Bienvenue Dinga, mkurugenzi wa huduma ya Kitaifa ya utabiri wa hali ya hewa Congo, amesema kuwa hilo ni tukio la kipekee zaidi tangu mafuriko makubwa ya Desemba mwaka wa 1961. 

Dkt. Dinga ambaye alihudhuria kikao cha Jopo la Uratibu wa Hali ya Hewa mjini Geneva, nchini Uswisi, amesema mvua kubwa ambazo ni mfano wa athari za El Niño, zilitabiriwa katika utabiri wa msimu wa Oktoba-Novemba-Desemba. 

Lakini ukosefu wa rasilimali na vifaa ulitatiza juhudi za kuokoa maisha na uwezo wa watu kuishi. “Tunahitaji kuimarisha mifumo yatahadhari ya mapema kulingana na mpango wa tahadhari kwa wote. Lakini tatizo ni ukosefu wa fedha. Tungekuwa na ufadhili, ingekuwa tofauti”. Amesema akiongeza kuwa mwaka wa 1995 kulikuwa na vituo 80 vya ufuatiliaji wa hali ya maji. Sasa viko 13 tu, kutokana na ukosefu wa fedha.

Jopo la Uratibu wa masuala ya maji la WMO 

Jopo la Uratibu wa masuala ya maji linasaidia na kushauri juu ya utoaji jumuishi wa shughuli zinazohusiana na maji za WMO kuhusiana na changamoto za sasa na zinazoibuka za kimataifa. 

Pia linafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya huduma za Hali ya Hewa na za maji na kukuza hatua za hali ya hewa.

Huduma hizo zinabainisha kwamba 

·         Hakuna anayeshangazwa na mafuriko.

·         Kila mtu yuko tayari kwa ukame.

·         Takwimu za hali ya hewa zinasaidia ajenda ya uhakika wa chakula.

·         Takwimu za ubora wa juu zinasaidia sayansi.

·         Sayansi hutoa msingi mzuri wa uendeshaji wa masuala ya maji.

·         Tuna ufahamu wa kina wa rasilimali za maji za ulimwengu wetu.

·         Maendeleo endelevu yanasaidiwa na habari za masuala ya maji

·         Ubora wa maji unapaswa kujulikana