Congo tekelezeni kimatendo sheria ya kulinda watu wa asili- Mtaalam

25 Oktoba 2019

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa jamii za asili, Victoria Tauli-Corpuz amehitimisha ziara yake ya siku  11 nchini Jamhuri ya Congo na kusisitiza umuhimu wa serikali kutekeleza kwa vitendo sheria ya kusongesha haki za jamii hiyo.

Katika ripoti yake iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, mwishoni mwa ziara yake hapo jana, mtaalamu huyo amesema anashukuru na kutambua hatua za serikali ya Congo ya kupitisha sheria namba 5 ya mwaka 2011 ya kuendeleza haki hizo ikiwemo za elimu, kijamii na hata umiliki wa ardhi lakini bado kuna changamoto kutokana na kusuaasua katika utekelezaji wa sheria hiyo iliyopitishwa mwaka 2015.

Amesema ingawa maafisa wa serikali wamekuwa mara kwa mara wakimhakikishia kuwa kuna utashi wa kisiasa wa kutekeleza sheria hiyo ambayo hata mwaka 2017 kulitolewa msururu wa maagizo ya kutekeleza, bado kuna vikwazo.

Bi. Tauli-Corpuz ametolea mfano ziara yake huko Kabo ambako kuna shule yenye wanafunzi wapatao 140 wa jamii ya asili, shule yenye walimu watatu ambao wote si wa jamii ya asili.

“Walimu wale walinijulisha kuwa wanalipwa mshahara wa dola 100 kwa mwezi lakini malipo hayo hata hawajalipwa kwa zaidi ya miezi 4 sasa na wakati wa miezi 3 ya likizo za shule pia hawalipwi. Nilishangazwa kusikia kuwa hata vitabu vyote vya mafunzo vinavyotumka shuleni vyote viko kwa lugha ya kifaransa na hii kwa mujibu wa walimu, uwezo wa watoto wa kutumia kifaransa katika darasa la tatu bado ni wa chini sana,” amesema mtaalamu huyo.

Mtaalam huyo amesema anaamini kuwa uwepo wa utashi wa kisiasa kutekeleza sheria hiyo ya kusongesha haki za jamii ya asili uende sambamba na kutenga bajeti ili kuweza kupata rasilimali zinazohitajika ili wapate haki zao.

“Nasisitiza tena mapendekezo yaliyotolewa na mtangulizi wangu kuwa mifumo ya kimsingi iliyowekwa ya kubagua watu wa jamii ya asili inahitaji ushiriki sahihi wa kijamii ili iweze kutambulika na hatua zichukuliwe ili kujenga heshima baina ya watu wa jamii zote nchini Congo,” amesema mtaalam huyo.

Amekumbusha kuwa kukabili changamoto hizo za elimu na nyinginezo kwenye afya na hata jamii hizo kushiriki kwenye miradi inayoweza kuathiri maeneo yao, kunaweza tu pale ambapo kuna juhudi za pamoja zikileta pamoja seriklai, mashirika ya kiraia na wadau wengine wa maendeleo na watu wenyewe wa asili.

“Watu wa asili hawapaswi kuonekana kuwa ni mzigo au kikwazo cha maendeleo au kuwa ni watu walio nyuma kimaendeleo. Wanapaswa kuchukuliwa kama binadamu wengine ambao wana utu na haki sawa kama wengine na waendelee na jukumu la kulinda mazingira yao,” amesisitiza Bi. Tauli-Corpuz

Amekumbusha kuwa wanaweza kuchangia maarifa yao ya asili katika usimamizi wa rasilimali asili, mabadiliko ya tabianchi na tiba za asili.

Wakati wa ziara hiyo inayotokana na mwaliko wa serikali, mtaalam huyo alikutana na viongozi wa serikali, mashirika ya kiraia, Umoja wa Mataifa na watu wa jamii ya asili.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter