Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yasaidia chanjo dhidi ya homa ya manjano Congo

Dozi moja ya chanjo dhidi ya homa ya manjano humpatia mtu kinga ya maisha dhidi ya ugonjwa huo hatari
WHO
Dozi moja ya chanjo dhidi ya homa ya manjano humpatia mtu kinga ya maisha dhidi ya ugonjwa huo hatari

WHO yasaidia chanjo dhidi ya homa ya manjano Congo

Afya

Nchini Jamhuri ya Congo, serikali kwa kushirikiana na shirika la afya duniani, WHO na wadau wengine wameendesha kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa ya manjano kwenye mji wa bandari wa Pointe Noire na maeneo ya jirani.

Zaidi ya watu milioni moja wenye umri wa kuanzia miezi Tisa walipatiwa chanjo katika kampeni hiyo ya siku sita iliyochochewa na kuthibitishwa kwa mgonjwa mmoja wa homa ya manjano tarehe 21 mwezi Agosti mwaka huu.

Kisa hicho kimoja ni kati ya visa shukiwa 200 tangu mwanzoni mwa mwaka huu ambapo Dkt. Ibrahima Socé Fall, mkurugenzi wa WHO barani Afrika akihusika na dharura amesema, Homa  ya manjano ni ugonjwa unaoibuka Afrika na watu milioni 400 hivi wako hatarini. Mwelekeo wetu ni kuzuia kabisa ugonjwa huo barani Afrika. Kwa hiyo Congo ni moja ya nchi 27 zilizo hatarini na tangu kisa kimoja kilipothibitishwa Pointe Noire tunaendesha kampeni kusaidia serikali kulinda raia walio hatarini kwa sababu homa ya manjano bado iko kwa kiwango kidogo Congo.”

 

Matairi yaliyotelekezwa hovyo ni mazingira bora ya mazalia ya mbu aina ya Aedes aegypti anayeeneza homa ya manjano
PAHO
Matairi yaliyotelekezwa hovyo ni mazingira bora ya mazalia ya mbu aina ya Aedes aegypti anayeeneza homa ya manjano

Ametaja vichochezi vya kuenea kwa homa hiyo barani Afrika kuwa ni kasi kubwa ya kupanuka kwa miji sambamba na usimamizi duni wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambayo huweka mazingira kwa mbu wanaoeneza ugonjwa huo kushamiri. Dkt. Ibrahima  ameongeza kuwa “Homa ya manjano ni ugonjwa unaoua lakini kwa bahati nzuri tuna chanjo thabiti ambayo inaweza kumpatia mtu kinga maisha yake yote. Kinga ya maisha, kwa hiyo kuchukua hatua haraka kumlinda kila mtu ni mkakati bora zaidi tunaoweza kutekeleza.”

Ugonjwa wa homa ya manjano unaenzwana mbu aina ya Aedes aegypti.

Kwa mujibu wa WHO mlipuko wa ugonjwa huo maeneo ya mijini hutia hofu kubwa.