Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

EmpowerU Cash+ yabadilisha maisha katika Wilaya ya Lamwo nchini Uganda

Jane Aciro wa kijiji cha Panyule – Agoro akipokea fedha kupitia mpango wa uhawilishaji fedha na UNICEF.
UNICEF/Maria Wamala
Jane Aciro wa kijiji cha Panyule – Agoro akipokea fedha kupitia mpango wa uhawilishaji fedha na UNICEF.

EmpowerU Cash+ yabadilisha maisha katika Wilaya ya Lamwo nchini Uganda

Msaada wa Kibinadamu

Mpango huo wa EmpowerU Cash+ ulikuwa unalenga idadi ya juu ya watoto kufikia wanne kwa kila kaya na kila mtoto kila mwezi alipewa Shilingi 45,000 za Uganda sawa na takribani  dola 11 za kimarekani hiyo ikimaainisha kila kaya ilipata jumla ya Shilingi za Uganda 180,000 sawa na takribani dola 47 za kimarekani kwa mwezi. Huduma hiyo ilikuwa kwa muda wa miezi sita katika wilaya za Lamwo, Adjumani, Yumbe, na Obongi lakini hapa ninaangazia wilaya moja tu, Lamwo. 

Huyu ni Gabriel Opala, mnufaika wa mradi huu wa EmpowerU Cash+, mkazi wa eneo la Olebi.  

Akionesha mguu wa mtoto wake mvulana mdogo, kovu limeanzia pajani hadi karibu na goti, anasema, “mtoto wangu alikuwa na tatizo la seli mundu katika mguu huu. Mguu ulikuwa unapinda na kuvimba. Nilitumia fedha nilizopata kutoka UNICEF kumpeleka mtoto hospitali kwa ajili ya upasuaji na sasa ninaweza kuona mabadiliko. Ninataka kuishukuru UNICEF kwa pesa niliyoipokea. Angalau sasa mtoto wangu anaweza kutembea. Sasa anaweza kwenda shule na kusoma kama watoto wengine.” 

Huyu ni Winnie Labol, naye mnufaika lakini yeye ni kutoka kijiji cha Polocire Mashariki, humohumo katika Wilaya ya Lamwo. Amembeba mtoto wake mchanga na anaeleza kwamba alipojifungua daktari alimwambia awe anakuja hospitali kila wiki kwa ajili ya matibabu. Labor aliitumia fedha aliyopewa na UNICEF kugharamia usafiri na tiba katika hospitali ya Lacor kwenye wilaya ya jirani ya Gulu.  

Na sasa tumsikilize Ajok Evelyn. Yeye kwa siku kadhaa aliumwa uchungu wa kujifungua na baadaye angalau akapata mtoto wa kike mwenye afya nzuri. Lakini likatokea tatizo. Sio kwa mtoto bali kwa mama. Akagundulika amepata tatizo la fistula. 

“Niliporudi nyumbani kutoka hospitali, sikuwa naweza kufanya kazi yoyote. Kibofu hakikuwa kimepona. Nilipokuwa ninakaa mkojo ulikuwa unanitoka.” 

Ajok alitumia pesa aliyoipata kutoka UNICEF akafanyiwa upasuaji wa kurejesha kibofu katika hali yake. Sasa anaishi maisha kawaida na ana uwezo wa kufanya shughuli zake za nyumbani.  

Fedha hizo pia zimeendeleza ujuzi kwa watu na hivyo kutengeneza njia kwa ajili ya shughuli za kuzalisha kipato endelevu. Pamela Abwoyo mkazi wa kijiji cha Apyeta ni shuhuda. 

“Ndoto yanngu ilikuwa kuanzisha biashara ya mapishi. Ndoto yangu imetimizwa na programu ya Mpower U. Nilitumia pesa kununua vitendea kazi. Tayari nimeanza biashara yangu. Ninataka kuwa na mgahawa wangu katika siku zijazo lakini kwa pesa kidogo ambazo Mpower U imenipatia, tayari nimewezeshwa. Asante kwa kuniwezesha.” 

Mradi huu haujaishia hapo, pia umekuza utamaduni wa kuweka akiba. Lucy Oyella alipopata pesa kutoka UNICEF akaiweka katika kundi lao la kuweka na kukopa…(Nats) Kama anavyoeleza, baadaye akaweza kukopa shilingi laki 4 za Uganda sawa na takribani dola 105 za kimarekani. Akanunua bidhaa kama nafaka, akauza akapata faida ya shilingi laki mbili za Uganda sawa na takribani dola 50 za kimarekani.  

Hakika ufadhili huu wa fedha taslimu kupitia UNICEF kwa kuungwa mkono na serikali ya Uholanzi na Uganda, umekuwa na mchango chanya wilayani Lamwo, kaskazini mwa Uganda.