Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nzige waliovamia Pembe ya Afrika hawahitaji viza kuingia nchi yeyote, wanashambulia tu:Lowcock

Nzige wa jangwani.
Picha: FAO/G.Tortoli
Nzige wa jangwani.

Nzige waliovamia Pembe ya Afrika hawahitaji viza kuingia nchi yeyote, wanashambulia tu:Lowcock

Msaada wa Kibinadamu

Janga la nzige limeendelea kuliathiri eneo la Pembe ya Afrika hasa Ethiopia, Kenya na Somalia, lakini sasa wameripotiwa pia kubisha hodi Uganda na huku nchi za Sudan Kusini na Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo katika tahadhari, kwa mujibu wa mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA.

Akizungumza kwenye kikao maalumu katika Umoja wa Mataifa hii leo kuhusu janga la nzige Bwana Mark Lowcock amesema “Ethiopia, Kenya na Somalia zimevamiwa na wimbi kubwa la nzige wa jangwani katika uvamizi mbaya zaidi wa nzige kwa kipindi cha miaka 70 nchini Kenya na miaka 25 nchini Ethiopia na Somalia.”

Bwana Lowcock amesema “wimbi moja la nzige waliozingira ukubwa wa kilometa moja , ambalo linajumuisha nzige milioni 40 hadi milioni 80, wanaweza kula kwa siku moja chakula ambacho kinatosheleza kulisha watu elfu 35.”

Pia amesema katika saa 24 zilizopita wimbi la nzige limevuka mpaka na kuingia Uganda. Ameongeza kuwa “Kama mjuavyo nzige ni wadudu wa kale sana ambao uhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine  na uvamizi wao unaweza kusambaratisha kabisa mazao na malisho haraka sana.”

Hali halisi

Mark Lowcock mkuu wa OCHA akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali nchini Yemen.
UN Photo/Manuel Elías
Mark Lowcock mkuu wa OCHA akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali nchini Yemen.

 

Akitolea mfano uvamizi wa nzige hao Kaskazini Mashariki mwa Kenya, amesema wimbi moja la nzige lilikadiriwa kuwa ni la ukubwa wa kilometa 2, 400 na nzige hao wanaweza kula chakula ambacho kinaweza kulisha watu milioni 84 kwa siku.

Amesema “nzige hao sio tu kwamba wana njaa lakini wanasafiri haraka sana, nzige hao hawahusiki na masuala ya uhamiaji, au kuhitaji pasi za kusafiria na wala hawaheshimu mipaka ya kimataifa . Hili ni tatizo la kikanda na tayari tumepokea taarifa za uharibifu mkubwa wa mazao na mimea katika kanda hiyo.”

Janga baada ya janga

Bwana Lowcock amesema wimbi hili la nzige limevamia Pembe ya Afrika ambayo tayari ilikuwa imeghubikwa na changamoto zingine kama ukame, njaa Somalia na Sudan Kusini, mafuriko na machafuko yanayoendelea hivyo imekuwa janga baada ya janga.

Uvamizi wa nzige unaweza kuathiri uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu.
Photo: FAO/Yasuyoshi Chiba
Uvamizi wa nzige unaweza kuathiri uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu.

 

Na watu milioni 30 hawana uhakika wa chakula katika eneo hilo la Pembe ya Afrika.

Kabla ya kukabiliana na tishio la sasa, Pembe hiyo ya Afrika imekumbwa na mahitaji makubwa yanayohitaji msaada wa kibinadamu ikiwemo suala la wakimbizi, wakimbizi wa ndani, utapiamlo, njaa na matatizo mengine.

Fedha zinazohitajika

Mkuu huyo wa OCHA amesema Ethiopia na Somalia kuna watu zaidi ya milioni 13 wanaohitaji msaada wa kibinadamu na kila nchi inahitaji dola bilioni moja ili kutatua changamoto hizo za kibinadamu kwa mwaka huu.

Katika eneo la Kaskazini mwa Kenya amesema “watoto huathirika na utapiamlo, Uganda ambako wimbi la nzige ndio limeingia hii inadhihirisha kwamba hatuwezi kumudu janga lingine ndio maana tunahitaji kuchukua hatua sasa kuepuka zahma kubwa zaidi na tunahitaji kuchukua hatua sasa “amesisitiza mkuu huyo wa OCHA.

Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa inastahili kushikamana ili kuepusha janga hili ikiwa ni pamoja na kulisaidia shirika la chakula na kilimo FAO ambalo linahitaji dola milioni 76 kupambana na janga la nzige.

Kisha Lowcock akatoa wito”Natoa wito kwa nchi husika, jumuiya ya kimataifa na wahisani kuongeza juhudi na kuongeza juhudi hizo za hatua sasa. Kuna hatari ya zahma kubwa na huenda tukaiepuka, tuna wajibu wa kujaribu, na tusipochukua hatua sasa basi tutakuwa na zahma kubwa.”