Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Sudan unaathiri maendeleo ya mashauriano kuhusu Abyei- UN

Martha Ama Akyaa Pobee (kwenye skrini), Msaidizi wa Katibu Mkuu katika kanda ya Afrika, Idara za Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani na Operesheni za ulinzi wa Amani, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Abyei.
UN Photo/Eskinder Debebe
Martha Ama Akyaa Pobee (kwenye skrini), Msaidizi wa Katibu Mkuu katika kanda ya Afrika, Idara za Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani na Operesheni za ulinzi wa Amani, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Abyei.

Mzozo Sudan unaathiri maendeleo ya mashauriano kuhusu Abyei- UN

Amani na Usalama

Hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejulishwa kuwa mzozo unaoendelea nchini Sudan unaweza kuathiri hali ya Abyei, eneo linalogombaniwa kati ya Sudan na Sudan Kusini. 

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika, Martha Ama Akyaa Pobee amesema hayo wakati Baraza hilo lilipokutana kujadili hali ya eneo hilo ambalo kwa sasa linasimamiwa na ujumbe wa mpito wa Umoja wa Mataifa kwenye eneo hilo, UNISFA. 

Maendeleo yaliyopatikana Abyei yako mashakani 

Bi. Akyaa Pobee amesema “licha ya maendeleo chanya yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kutolewa kwa ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu Abyei, mlipuko wa mapigano nchini Sudan unaweza kuwa na athari hasi kwenye fursa ya maendeleo ya kisiasa huko Abyei, halikadhalika masuala ya mpaka.” 

Bi. Pobee ameongeza kuwa huku mapigano yakiendelea na harakati za mashauriano nazo zikipamba moto, Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia Sudan Kusini na Sudan pindi mashauriano kuhusu Abyei yatakapoanza tena. 

Kwa mujibu wa Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya Afrika, “hali ya kibinadamu huko Abyei bado inakabiliwa na changamoto kwani Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanapatia  msaada wa kiutu kwa watu 212,000 walioko hatarini zaidi Abyei wakiwemo wakimbizi wa ndani wapatao 30,000.” 

Mapigano ya kikabila yameshamiri Agok 

Katika kipindi hiki cha mwaka mzima ambacho Bi. Pobee ametolea tathmini ya hali ya usalama amesema mapigano ya kikabilia yamekwamisha juhudi za kusambaza misaada ya kibinadamu, ambapo baadhi ya mashirika yamelazimika kuondoka eneo la Agok kufuatia mapigano mwezi Februri mwaka huu ambapo watumishi wawili wa kiutu waliuawa wakati wa shambulio huko Rumamier tarehe 2 mwezi huo wa Februari. 

Naye Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Pembe ya Afrika, Hanna Serwaa Tetteh, alipata fursa ya kuhutubia Baraza la Usalama akisema, “mapigano yaliyoibuka Sudan tarehe 15 mwezi Aprili mwaka huu katika jeshi la serikali, (SAF) na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), pamoja na kuathiri wasudan, pia yanaathiri vibaya uhusiano kati ya Sudan na Sudan Kusini. 

Usalama wa kiutu, kiuchumi na kijamii mashakani 

Kwa mujibu wa Tetteh, “usalama wa kibinadamu, na athari za kiuchumi na kijamii kutokana na kinachoendelea Sudan vimeibua hofu miongoni mwa viongozi wa kisiasa nchini Sudan Kusini. 

 “Kuna uwezekano wa wakimizi zaidi ya 200,000 waliokuwa wanapata hifadhi Sudan, kurejea nyumbani Sudan Kusini iwapo amani haitarejea haraka iwezekanavyo Sudan,” amesema Mjumbe huyo Maalum wa Katibu Mkuu wa UN. 

Bi. Tetteh amesema iwapo hilo litatokea basi itakuwa changamoto kubwa sana kwa taifa hilo ambalo theluthi mbili ya raia wake tayari wanahitaji msaada wa kibinadamu, kwa sababu hivi sasa mamlaka za Sudan haziwezi kudhibiti mipaka yake kwa ufanisi. 

Jamii ya kimataifa iimarishe wito wa usaidizi 

Na kwa kuzingatia hilo, hali ya ukosefu wa usalama kwenye mipaka ya Sudan na Sudan Kusini inaweza kuongezeka kutokana na mienendo ya vikundi vilivyojihami huko mpakani sambamba na magenge ya uhalifu. 

Sudan na Sudan Kusini nazo zapaza sauti 

Mwakilishi wa Kudumu wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Al-Harith Idriss Al-Harith Mohamed akihutubia mkutano huo amesema“tungependa kusisitiza ya kwamba hali ya Abyei haiwezi kukumbwa na madhara yoyote kutokana na kinachoendelea Sudan, na kwamba hili limesisitizwa katika mikutano ya hivi karibuni kati ya nchi zote mbili.” 

Bwana Mohamed amesema suala ni kwamba nchi yake imejizatiti kupata suluhisho kwa njia ya amani kwenye mzozo wa sasa ulioanzishwa na kundi la waasi dhidi ya jeshi lililojihami. 

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Sudan Kusini kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Akuei Bona Malwal, amesema “mkutano huu wa leo umefanyika wakati Sudan inapitia kipindi kigumu ijapokuwa uhusiano kati ya nchi mbili hizi ni mzuri na unasalia hivyo, licha ya changamoto zinazoendelea kati ya pande kinzani.” 

 Balozi Malwal ametamatisha hotuba yake kwa kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuimarisha wito wao wa kusongesha hali ya kiutu ndani ya Sudan na nchi Jirani zilizopokea wakimbizi ndani ya siku chahe bila kujiandaa mara tu baada ya mapigano kuzuka kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum na maeneo mengineyo. 

Mwezi Juni mwaka 2011, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio kwa mara ya kwanza kuanzisha uwepo wa jeshi la mpito la Umoja wa Mataifa kwenye eneo hilo la Abyei linalozozaniwa kati ya Sudan na Sudan Kusini.