Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni kwa vipi mfumo wa wamasai kujikwamua unaweza kuwa mfano kwa wengine Afrika?

Dkt. Venance Shillingi, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe nchini Tanzania akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kando mwa mkutano wa UN na wanazuoni uliofanyika New York, kuanzia Desemba 5-7 2023.
UN/Assumpta Massoi
Dkt. Venance Shillingi, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe nchini Tanzania akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kando mwa mkutano wa UN na wanazuoni uliofanyika New York, kuanzia Desemba 5-7 2023.

Ni kwa vipi mfumo wa wamasai kujikwamua unaweza kuwa mfano kwa wengine Afrika?

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kitendo cha kabila la jamii ya wamasai kuweza kujimudu na maisha hata baada ya ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kuvuruga upatikanaji wa malisho kwa ajili ya mifugo yao kimeonekana kama moja ya mbinu mujarabu zinazoweza kusaidia nchi za Afrika kujengea mnepo wananchi wapo pindi mbinu walizozoea kujipatia kipato zinapovurugika.

Mbinu hizo zinazotumiwa na wamasai hususan nchini Tanzania zimeripotiwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro, mashariki mwa Taifa hilo la Afrika MAshariki, Dkt. Venance Shillingi wakati akizungumza na Idhaa ya Kiswahili  ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani baada ya mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu Afrika, OSAA.

Dkt. Shillingi alikuwa ni mmoja wa wanazuoni walioshiriki kwenye mkutano huo wa siku tatu uliokuwa unamulika ni kwa vipi bara la Afrika linaweza kukabili changamoto za kiuchumi, kijamii, haki na amani kwa kutumia majawabu yatokanayo na bara lenyewe badala ya majawabu ya kuletewa, ikiwemo kuangalia majawabu ambayo tayari yanatumiwa kama vile wamasai.

Wamasai na mbinu mpya za kujipatia kipato

“Nilitaka niangalie kuhusu wamasai wa huko Kilosa mkoani Morogoro ambao wao ni wafugaji lakini kuna changamoto ya hali ya hewa kubadilika badilika. Mfano ukame wa mara kwa mara na wao ni wafugaji wa ng’ombe, yaani bila ng’ombe hakuna maisha. Kwa kuwa eneo lao lina miradi mingi mfano ule reli ya mwendo kasi, SGR,  ikabidi waone ni kwa vipi utamaduni wao unaweza kuwasaidia vipi kuja na miradi mingine ya kuwawezesha kuishi,” amesema Dkt. Shillingi akifafanua utafiti wake atakaofanya.

Amesema kwenye SGR suala la  ulinzi kuanzia Dar es salaam hadi Dodoma na kuendelea ni wamasai na wamechukuliwa vile “kwa sababu ya uimara wao kulingana na tabia zao, uwezo wao wa kulinda kama mamorani kulinda familia zao. Kwa hiyo zile mbinu zimewasaidia wao kuajiriwa wapate kipato kingine kutokana na ajira. Lakini wanapopata kipato chao kutokana na ajira wananunua ng’ombe.”

Jamii ya wamasai imeendelea kuhifadhi si tu lugha yake bali pia tamaduni, ingawa mabadiliko ya maisha yanatishia tamaduni na mila.
ILO/Marcel Crozet
Jamii ya wamasai imeendelea kuhifadhi si tu lugha yake bali pia tamaduni, ingawa mabadiliko ya maisha yanatishia tamaduni na mila.

Dkt. Shillingi amesema wengine ambao hawako kwenye SGR, wanakwenda kwenye miji mikubwa na kuingia kwenye kazi ya kusuka nywele, kwani ususi ni stadi ambayo wamefundishwa kutokana na mila na tamaduni zao.

Mhadhiri Mwandimizi huyo wa Chuo Kikuu Mzumbe anatanabaisha, “utafiti wangu nauunganisha ya kwamba nchi zetu za Afrika zijifunze kwenye utamaduni wa kabila la wamasai ili tuweze kuheshimu mila na tamaduni zetu ili ziweze kutuvusha.”

Amesema wamasai licha ya changamoto za ukame, kugombania ardhi na wakulima, bado wameimarika.

Kwa mantiki hiyo utafiti wake hatma yake ni kudadavua ni kwa vipi stadi au elimu wanayopatiana jamii ya wamasai imeweza vipi kuwakinga au kuwajengea mnepo na changamoto zinazoibuka hivi sasa.

Mitaala ya elimu nayo pia imulikwe

Katika mkutano huo pia Dkt. Shillingi anasema walimulika mitaala ya elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi Vyuo Vikuu ambapo kwa kiasi kikubwa elimu inayotolewa kama vile Tanzania inalenga watoto wa nchi nzima. 

“Tunapendekeza kwamba elimu iendane na eneo husika ili mwanafunzi aweze kujipatia kipato katika ngazi yoyote ile anayohitimu masomo. Mfano kama mtoto yuko Arusha, afundishwe lugha zaidi ya moja ya kigeni,” amesema Dkt. Shillingi akieleza kuwa, mkoa wa Arusha unajulikana kwa utalii, hivyo mtoto akimaliza hata darasa la Saba ataweza kujipatia kipato kwa kuwa na elimu ya kuongoza utalii.

Dkt. Shillingi amesema utafiti wake utakapokamilika utachapishwa lakini vile vile wataandaa andiko la kisera kwa ajili ya wenye mamlaka, andiko likiwa na mapendekezo ya hatua za kuchukua kama mchango wa wanazuoni katika kufanikisha maendeleo endelevu Afrika.