Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanasiasa wakishikamana na wananchi na FAO tutadumisha uhakika wa chakula sudan Kusini: Malo

Meshack Malo mwakilishi wa FAO nchini Sudan Kusini Akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa mataifa.
UN News
Meshack Malo mwakilishi wa FAO nchini Sudan Kusini Akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa mataifa.

Wanasiasa wakishikamana na wananchi na FAO tutadumisha uhakika wa chakula sudan Kusini: Malo

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Uhakika wa chakula ni moja ya changamoto kubwa katika maeneo yenye mizozo duniani kutokana na kutokuwepo kwa usalama na watu kufurushwa makwao hali inayofanya kuwa vigumu kwa wakulima kutekeleza wajibu wao. 

Kwa kulitambua hilo shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limekuwa msitari wa mbele kwa miradi mbali mbali ya kuwasaidia wakulima na wafugaji kwenye mizozo ili kuhakikisha wanapunguza mzigo wa kuwa tegemezi wa msaada wa chakula.

Soundcloud

Moja ya nchi ambako FAO imejikita na miradi hiyo ni Sudan Kusini ambako vita bado inaendelea katika maeneo mbalimbali. 

Akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa hii Meshack Malo mwakilishi wa FAO nchini humo amesema FAO ina miradi mingi ambayo inawasaidia wakulima wa taifa hilo “ Kutokana na vita kuha hitaji kubwa sana la msaada wa chakula hivyo Fao inafanyakazi kubwa sana kuhakikisha kwanza inaongeza mazao ukizingatia kwamba hivi sasa takriban asilimia 4 pekee ya nchi ndio kuna kilimo, pili tunaangalia afya ya wanyama, wakulima Sudan Kusini wanapenda sana mifugo hasa ng’ombe na ndio pia huwa kichocheo cha vita kwani kuna watu milioni 12 lakini wanyama ni karibu milioni 36,  ya tatu ni uvuvi, sababu ya kuwepo kwa mto Nile ambao ni mkubwa sana kuna fursa kubwa ya uvuvi wa samaki hapa Siudan Kusini na mwisho ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri sana taifa hilo hivyo shirika letu linafanyakazi na serikali kuhakikisha wakulima wanabadili mienendo yao ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”

Nchini Sudan Kusini, mama akiwapa watoto wake uji wa mtama.
FAO/Stefanie Glinski
Nchini Sudan Kusini, mama akiwapa watoto wake uji wa mtama.

Nani walengwa wa miradi hii ya FAO

Bwana Malo amesema walengwa wakubwa wa miradi hii ni wanawake kwa kuwa wao ndio waathirika wakubwa wa machafuko na ndio wanaofurushwa mara kwa mara vita inapozuka.

Hata hivyo amesema kwa kutambua nafasi walioyonayo vijana katika jamii ni kundi lingine ambalo wanalilenga.

“Kwa sababu ya vita Sudan Kusini wanawake ndio wanaoshughulika sana na kilimo hivyo tunawalenga zaidi wanawake lakini kwas asa tunajaribu kuwaleta sana vijana kwa sababu vijana kwasababu hawabobea sana katika kilimo , wanaona hakina faida, hakina pesa na hakivutii hivyo tuna kazi kubwa ya kuwahamasisha na kuwalenga vijana katika kilimo kile ambacho kinaweza kuwavutia.”

Changamoto gani zinawakabili katika kutimiza lengo lenu?

Kutokana na vita inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Sudan Kusini Bwana Malo anasema “Changamoto kubwa hapa ni hali ya usalama kwani vita bado inaendelea na kama ujuavyo ukulima unahitaki hali tulivu ya usalama ili wakulima waweze kulima, kuangalia mazao yao na kuvuna .”

Lakini amesema mara nyingi utakuta machafuko yanawalazimisha wakulima kufungasha virago na kukimbia kutoka eneo moja kwenda kwingine kusaka usalama na hivyo kuathiri shughuli za kilimo Sudan Kusini.

Ili kupunguza changamoto hii amesema, “Tunaendelea kuwahisi wanasiasa na kuwakumbusha kuwa usalama w anchi utaendelea kuimarisha sekta ya kilimo na ndio maana hata kama eneo letu ni masuala ya chakula tunafanyakazi pamoja na wanasiasa ili kuhakikisha usalama.”

Mbali ya usalama ametaja changamoto niyine kubwa ya pili kuwa ni “Fedha na kwa sababu ya vita hakuna barabara na wakati mwingine tunalazimika hata zile mbegu tunazogawa kwa wakulima tunazibeba kwa Ndege ambayo ni gharama kubwa.”

Pia amesema vita katika nchi jirani ya Sudan nayo imeongeza changamoto kwani raia wa sudan Kusini waliokuwa wakifanyakazi Sudan wengi wamelazimika kurejea nyumbani na hali ya uchumi kwa ujumla imeendelea kuathiri kazi za Fao nchini humo.

Margerita, Mwanamke mkulima nchini Sudan Kusini, anapanda mbegu za zao la mahindi kwa mwaka ujao.
FAO/Jean Di Marino
Margerita, Mwanamke mkulima nchini Sudan Kusini, anapanda mbegu za zao la mahindi kwa mwaka ujao.

Je kuna mafanikio yoyote hadi sasa ?

Baada ya wanasiasa nchini Sudan Kusini kuja pamoja miaka mitatu iliyopita Malo anasema “Ufanisi umeanza kupatikana, hasa katika uzalishaji wa chakula ambapo kwa sasa unakuta kile kiwango cha chakula ambacho Sudan Kusini inaweza kujimudu yenyewe mwaka jana kilifikia kama miezi mitano na nusu.”

Hata hivyo amesema hiyo ni hatua nzuri kalini haitoshelezi hivyo lengo lao kubwa ni “Tukiweza kusukuma zaidi na hali ya usalama iongezeke kwa mwaka huu ili msaada wa chakula usalie kama miezi mitano au minne pekee hayo yatakuwa mafanikio makubwa kwetu, lakini hadi sasa tulifanikiwa kupata chakula cha kutosha miezi mitano na nusu pekee.”

Pia amesema kwa kuzingatia kwamba mwaka huu kuna uchaguzi mkuu nchini Sudan Kusini wanaendelea kuhimiza suala la Amani ili mafanikio yaliyopatikana yasije rejeshwa nyuma.

“Tunaendelea kuwaomba na kuwasihi wanasiasa kuwa uchaguzi usije ukaharibu yake maendeleo yaliyopatikana hadi wakati huu.”

Nini wito wako kwa wananchi na kwa jumuiya ya kimataifa?

Bwana Malo amesema “Kwanza kwa jumuiya ya kimataifa nawaomba waweze kuipatia hii nchi nafasi, wasife moyo na tuna imani kuwa nchi hii itaendelea..”

Na kwa wananchi wa Sudan Kusini amesema “Haswa kwa wanasiasa wakiweza kuweka vichwa vyao pamoja na kuweza kufanyakazi pamoja wakiwafikiria wananchi wa kawaida , basi ile mistari mirefu ya watu kupanga kupata mgao wa chakula itapungua.”

Amesema ni muhimu kwa wanasiasa kushikamana na kuhakikisha siasa nzuri ili nchi iweze kuendelea mbele.