Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Jamhuri ya Congo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, UN kusaidia

Usaidizi wa dharura kwa waathirika wa mafuriko nchini Kongo.
WHO
Usaidizi wa dharura kwa waathirika wa mafuriko nchini Kongo.

Mafuriko Jamhuri ya Congo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, UN kusaidia

Tabianchi na mazingira

Mafuriko yaliyoenea kutokana na mvua kubwa isiyo ya kawaida katika Jamhuri ya Congo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) yamesababisha athari kubwa kwa watu na mali zao. 

Congo Brazzaville 

Kutoka katika mji mkuu Brazzaville, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) limeripoti leo kwamba kwa upande wa Jamhuri ya Congo, mafuriko yamesababisha zaidi ya watu 336,000 kuhitaji msaada wa haraka wa kibinadamu. Mafuriko hayo pia yameharibu vituo vya afya na shule na kuzamisha maeneo ya mashambani. 

Maeneo tisa kati ya 12 za nchi hiyo zimeathirika, huku maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo pamoja na maeneo yanayopakana na Mto Congo yakiwa miongoni mwa yaliyoathiriwa zaidi. Kulingana na makadirio ya wataalam, mvua ya sasa ni mara mbili ya wastani wa iliyorekodiwa katika msimu wa mwaka 2022-2023. Kiwango cha maji katika Mto Ubangi, mkondo mkubwa wa ukingo wa kulia wa Mto Congo, kimefikia kiwango cha juu kabisa. 

Mafuriko hayo yameharibu vituo 34 vya afya, shule 120 na zaidi ya nyumba 64,000 katika maeneo yaliyoathiriwa. Mahitaji ya kibinadamu yanakadiriwa kuongezeka, na hivyo kuzidisha hali mbaya ya watu walioathiriwa, hasa jamii zilizo hatarini. 

"WHO imejitolea kuunga mkono serikali kuongeza hatua za dharura kuokoa maisha na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za kimsingi," anasema Dkt. Lucien Manga, Mwakilishi wa WHO katika Jamhuri ya Congo na anaongeza kwamba wanashirikiana na mashirika washirika ili kuimarisha mwitikio wa misaada, kusaidia maisha na kupunguza tishio la milipuko ya magonjwa." 

Tishio kuu la kiafya ni pamoja na hatari ya milipuko ya magonjwa yanayosambazwa na maji kama vile kipindupindu, magonjwa yanayoenezwa na wadudu kama vile malaria au dengue, na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kama vile surua. Lishe ya afya ya mama na mtoto pia iko hatarini, wakati unyanyasaji wa kingono na kijinsia unaweza pia kuongezeka. Ukosefu wa uhakika wa chakula, lishe, upatikanaji wa huduma za afya, pamoja na maji salama, huduma za usafi wa mazingira na huduma za usafi huenda zikazorota. Kuhakikisha mwendelezo wa utunzaji wa magonjwa sugu kama VVU au kisukari na afya ya akili, huku ukipunguza hatari ya kuzama na majeraha bado ni muhimu. 

Mpango wa kukabiliana na dharura wa sekta mbalimbali unatayarishwa ili kusaidia watu walioathirika, ikiwa ni pamoja na kutoa chakula na pembejeo za kilimo ili kusaidia maisha na kuboresha usalama wa chakula; matibabu ya utapiamlo miongoni mwa watoto chini ya miaka 5, kutoa huduma bora za afya kwa wajawazito na wanaonyonyesha; pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira. 

Kwa kushirikiana na wadau, WHO inaongeza juhudi za kutoa huduma za afya za dharura ili kuepusha kuenea kwa magonjwa; dawa muhimu na vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha; na kuhakikisha huduma muhimu za afya kupitia vituo vya afya vinavyofanya kazi na kliniki zinazohama. 

WHO pia inaisaidia Wizara ya Afya ya Umma katika kuweka tahadhari ya mapema na mfumo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, pamoja na kupeleka haraka timu yake ya kitaifa ya watoa huduma wa kwanza kwa uchambuzi wa hali ya haraka ili kuhakikisha shughuli za usaidizi zinazofaa. 

“Juhudi pia zinafanywa ili kuhakikisha kuwa masomo yanaanza tena chini ya hali zinazofaa katika maeneo yaliyoathirika pamoja na utoaji wa msaada wa kisaikolojia kwa watoto na kutoa huduma za ulinzi, ikiwa ni pamoja na kuzuia ukatili wa kijinsia na matunzo kwa wahasiriwa.” Imeeleza taarifa hiyo ya WHO. 

Congo Kinshasa 

Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York katika Mkutano wake na waandishi wa Habari ameeleza kuwa kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kufuatia mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi ambayo yameathiri karibu nusu ya majimbo ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na Kinshasa, leo, wafanyakazi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) na wadau wa misaada ya kiutu wamekutana na Waziri wa Masuala ya Kibinadamu wa nchi hiyo ili kujadili mpango wa kuchukua hatua na kutembelea maeneo yaliyoathirika mjini Kinshasa.  

“Mpango wa kitaifa wa kukabiliana na maafa ulioandaliwa na Serikali unakamilishwa, kwa uratibu wa sisi wenyewe na wadau wake.” Ameeleza Stéphane Dujarric. 

Ziara ya pamoja katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko mjini Kinshasa imepangwa kufanyika kesho, 13 Januari. 

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza akisema, “Washirika wetu wa misaada ya kiutu wanasaidia shughuli za msaada wa dharura katika baadhi ya maeneo, hasa Kivu Kusini na Tanganyika, ikiwa ni pamoja na afya, maji, usafi na usafi wa mazingira. Lakini kwa majimbo mengi, jitihada za kukabiliana nazo zinatatizwa na rasilimali chache, ukosefu wa uwezekano wa tathmini, na uwepo mdogo wa wafanyakazi wa misaada. 

Mahitaji makubwa ni chakula, maji, malazi, vyoo, huduma za ulinzi, huduma za afya, na kuzuia malaria. 

Wafanyakazi wa usambazaji misaada wanashambuliwa 

Wakati huo huo, wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wanaendelea kushambuliwa katika eneo la mashariki mwa nchi. Mapema mwezi huu wa Januari tarehe 4, katika eneo la Djugu, huko Ituri, watu wenye silaha walishambulia lori lililokuwa na chakula cha WFP. Liliharibika na kukwama barabarani. Lori lilichomwa, na chakula kilichokuwa kikisafirishwa hadi Bunia kiliporwa, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaeleza waandishi wa habari.

Pia, katika jimbo la Ituri, walinzi wa amani walituma doria huko Panza jana kujibu mashambulizi kati ya kundi la waasi la CODECO na wanamgambo wa Zaire. 

Kufuatia mapigano hayo, raia walitafuta hifadhi na ulinzi karibu na kituo cha muda cha MONUSCO huko Drodro, ambacho kiko karibu na Djugu. 

MONUSCO inafuatilia hali ilivyo na walinda amani wanaendelea kushika doria katika eneo hilo hadi hali itakapotengemaa.