Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Grace Mukamana (kushoto) na mkulima mwingine nchini Rwanda wakitumia simu kupata taarifa za hali ya hewa.

IFAD: Mifumo ya utoaji maonyo mapema dhidi ya hali ya hewa yajengea mnepo wakulima wadogo

©IFAD/Simona Siad
Grace Mukamana (kushoto) na mkulima mwingine nchini Rwanda wakitumia simu kupata taarifa za hali ya hewa.

IFAD: Mifumo ya utoaji maonyo mapema dhidi ya hali ya hewa yajengea mnepo wakulima wadogo

Tabianchi na mazingira

Mabadiliko ya tabianchi yanafanya matukio ya hali mbaya ya hewa kuwa makali zaidi na ya mara kwa mara. Mifumo ya utoaji maonyo mapema  ambayo ni sahihi, rahisi kutumia na kutoa taarifa sahihi kuhusu hali ya hewa husaidia kupunguza vifo na hata kupotea kwa njia za kujipatia riziki au kipato.

 

Kwa kupatiwa maonyo ya mapema, wakulima wadogo wanakuwa na muda unaotakiwa wa kuhifadhi salama mazao yao, wanyama na kujiandaa kwa maafa. Hata wakati ambapo uharibifu fulani hauwezi kuepukika, inakuwa rahisi kurejesha maisha ya kawaida kwa jamii iliyoathirika.

Ingawa hivyo, ni nusu tu ya nchi zenye maendeleo duni duniani, au LDCs na asilimia 39 ya nchi za visiwa vidogo zinazoendelea zilizoko kwenye mazingira hatarishi, ndio zenye mifumo ya tahadhari za mapema  Cha kushangaza, huko ndiko mifumo hiyo inahitajika zaidi kwani  zinakabiliwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

Kichocheo cha mafanikio

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD unabadilisha hali hii kwa kuwezesha watu wa vijijini kupata kwa wakati taarifa sahihi za hali ya hewa na kuwawezesha kukabiliana na dhoruba inayokuja.

IFAD inasema kwa miaka mingi wamejifunza kwamba:

 Mifumo fanisi ya taarifa za hali ya hewa inategemea wadau, kuanzia wanasayansi, watunga sera hadi wafanyakazi wa ugani vijijini. Kila mtu lazima achangie na kuendeleza mapendekezo mahsusi kwa watu wa vijijini.

Wakulima na jamii, wakiwemo wanawake na vijana, lazima washirikishwe katika kubuni na kuzalisha mifumo ya taarifa za hali ya hewa inayowafanyia kazi.

Mafunzo ni muhimu ili kuzalisha, kuelewa, kuwasilisha na kutumia data kwa ufanisi.

Hadithi za mafanikio kutoka kote ulimwenguni zinaonesha jinsi IFAD inavyotumia mafunzo haya, ili wakulima na wafugaji wanufaike na mifumo ya tahadhari ya mapema.

Grace Mukamana mkulima nchini Rwanda hupokea taarifa kuhusu tabianchi kupitia simu yake ya kiganjani au rununu.
©IFAD/Simona Siad
Grace Mukamana mkulima nchini Rwanda hupokea taarifa kuhusu tabianchi kupitia simu yake ya kiganjani au rununu.

Kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi nchini Rwanda

Kwa miaka kadhaa, Grace Mukamana, mkulima nchini Rwanda alikumbana na changamoto nyingi katika ukulima wa mahindi, maharagwe na buni, mashariki mwa nchi, huku hali ya hewa ikizidi kuwa mbaya na kuendelea kuharibu mavuno yake.

Kwa hivyo wakati mradi wa IFAD wa kusaidia wakulima kudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno na kilimo biashara au PASP, ulipoanzisha huduma za hali ya hewa katika kijiji chake, Grace alijiunga. 

Grace alifundishwa kutafsiri mienendo ya kihistoria ya hali ya hewa na kuchanganya maarifa ya kisayansi na uzoefu wake mwenyewe ili kuchagua mbegu zinazofaa, kujiandaa kwa mahitaji ya kuhifadhi na kusindika, na kuwekeza katika bima ya mazao. Anapata taarifa za hali ya hewa mara kwa mara kupitia ujumbe wa simu ya kiganjani au rununu, SMS ili aweze kufanya maamuzi sahihi kwa shamba lake.

Tangu ajiunge na mradi huo, Grace ameona maisha yake yamebadilika. Pamoja na mazao yake ya kilimo kuongezeka maradufu, anaweza kulisha familia yake na kupeleka watoto wake shule.

Akiwa amejilinda kwa kupata data za tabianchi, Bwana Le (katikati) anaweza kulinda makonde yake ya mpunga dhidi ya ongezeko la kina cha maji ya bahari nchini Viet Nam.
©IFAD
Akiwa amejilinda kwa kupata data za tabianchi, Bwana Le (katikati) anaweza kulinda makonde yake ya mpunga dhidi ya ongezeko la kina cha maji ya bahari nchini Viet Nam.

Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Viet Nam 

Katika eneo la bonde la mto Mekong nchini Viet Nam, makonde ya mpunga yenye rangi ya zumaridi-kijani yanazidi kutishiwa na ongezeko la kina cha maji ya bahari, maji ambayo yanaingiza maji ya chumvi kwenye maji ya mto yasiyo na chumvi.

Lakini kwa kutelezesha kidole kwa urahisi kwenye skrini ya simu janj, wakulima wa mpunga kama Le Hoang Ro wanaweza kupata data za kuaminika za eneo lake kuhusu viwango vya chumvi kutoka mtandao wa kufuatilia maboya na kuchukua hatua.

Bw. Le mshiriki wa mradi wa IFAD wa kuwezesha wakulima kuhimili mabadiliko ya tabianchi au AMD anasema, "ninapojua kiwango cha chumvi kwenye maji ni kikubwa, mimi huhifadhi maji kwenye bwawa langu na kisha kufunga kalvati ili kuzuia maji ya chumvi yasiingie shambani mwangu."

Katika maeneo ya ndani zaidi nchini Kyrgyzstan, mifumo ya utoaji maonyo mapema kuhusu hali ya hewa inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha.
IFAD
Katika maeneo ya ndani zaidi nchini Kyrgyzstan, mifumo ya utoaji maonyo mapema kuhusu hali ya hewa inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha.

Mifumo ya tahadhari ya mapema nchini Kyrgyzstan

Katika mabonde na milima mirefu ya Kyrgyzstan, wafugaji hutumia mfumo wa taarifa za mabadiliko ya tabianchi uliotengenezwa kwa usaidizi mradi wa pili wa IFAD wa kuendeleza mifugo na masoko, au LMDP-II ili kupata onyo la mapema la hatari zitokanazo na hali ya hewa, kama vile mvua ya mawe au theluji kali.

Tangu mwaka 2019, maonyo 11 kuhusu hatari na majibu yaliyopendekezwa yalitolewa siku 10 mapema kupitia tovuti.

Karybek Karabaev ni Mkuu wa kikundi cha jamii cha wenyeji kinachosimamia mfumo wa ikolojia tete ambao wafugaji hutegemea. Yeye na wenzake wanajua jinsi ya kutathmini hatari na huwapigia simu wafugaji ili kuwasaidia kupanga njia za kupita kwa ajili ya malisho ya mifugo yao. Kwa njia hii, hata wafugaji katika mikoa ya mbali zaidi wanapata maonyo ya kutosha juu ya hali mbayá ya hewa.

Maonyo ya mapema, na ujuzi na uwezo wa kuyafanyia kazi, vinaweza kuleta tofauti kati ya mbinu za kujipatia kipato zilizoharibiwa na mnepo. Kwa usaidizi wa IFAD, watu wa vijijini kote ulimwenguni wanapata mbinu na maarifa wanayohitaji kukabiliana na dhoruba.

Kusoma zaidi taarifa kutoka IFAD kuhusu huduma kuhusu tabianchi bofya hapa