Pande kinzani Kyrgyzstan jizuieni na machafuko zaidi- Guterres 

6 Oktoba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa pande husika katika mvutano wa baada ya uchaguzi wa bunge nchini Kyrgyzstan kujizuia na machafuko zaidi baada ya taarifa za watu kujeruhiwa na mmoja kupoteza maisha katika maandamano yaliyozuka jana Jumatatu. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake Bwana. Guterres amesema amesikitishwa na kifo kilichotokea na majeruhi na kutaka hatua zote zichukuliwe kulinda maisha ya watu. 

Maandamano hayo ya jana yamefuatia uchaguzi wa bunge uliofanyika tarehe 4 Oktoba ambao umezusha mvutano.  

Kwa mujibu wa duru za habari uchaguzi huo unatarajiwa kurudiwa lakini kwa maandamano yanayoendelea mitaani na kila upande rais wa sasa na kiongozi wa upinzani kujitangazia ushindi ni vigumu kusema nani atakayeandaa ujaguzi huo wa marudio au kuongoza taifa hilo la asia ya Kati hadi wakati huo. 

Marais wawili wameshawahi kuondolewa madarakani kwa njia hii ya maandamano na machafuko nchini Kyrgyzstan katika miaka 15 iliyopita. 

Katibu Mkuu amezichagiza pande zote nchini humo kujihusisha katika majadiliano na kukubaliana hatua itakayofuata kwa kuzingatia katiba. 

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia juhudi zenye lengo la kupata suluhu ya amani ya hali ya sasa ikiwemo kupitia kituo cha kikanda cha Umoja wa Mataifa kwa ajili ya masuala ya diplomasia kwa nchi za Asia ya Kati (UNRCCA).
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud