Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshindi wa jumla wa tuzo ya Nansen 2019 atangazwa, anatoka Kyrgyzstan

Azizbek Ashurov, mwanasheria from Kyrgyzstan, amechaguliwa kama mshindi wa tuzo ya Nansen mwaka wa 2019 itolewayo na shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR.
UNHCR/Chris de Bode
Azizbek Ashurov, mwanasheria from Kyrgyzstan, amechaguliwa kama mshindi wa tuzo ya Nansen mwaka wa 2019 itolewayo na shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Mshindi wa jumla wa tuzo ya Nansen 2019 atangazwa, anatoka Kyrgyzstan

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakili kutoka nchini Kyrgyzstan, Azizbek Ashurov ameibuka mshindi wa jumla wa tuzo ya mwaka huu ya Nansen inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kutokana na jitihada zake za kutokomeza ukosefu wa utaifa nchini mwake.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa hii leo imesema Ashurov kupitia shirika lake la mawakili bila mipakaka, Ferghana Valley Lawyers Without Borders (FVLWB), amesaidia zaidi ya watu 10,000 nchini Kyrgyzstan kupata utaifa wa taifa hilo kufuatia kuvunjika kwa uliokuwa umoja wa kisovieti.

Miongoni mwao ni watoto 2,000 ambao sasa watakuwa na haki ya kupata elimu na mustakabali ulio na uhuru wa kusafiri, kuoa, kuolewa na hata kufanya kazi.

Wakati wa zama za Usovieti, kulikuwa hakuna mipaka na watu walikuwa na uwezo wa kusafiri kwenye eneo hilo la Asia ya Kati bila nyaraka zozote na kuweza kupata vibali vya ukazi na kuoa au kuolewa.

Hata hivyo baada ya kuvunjika kwa umoja wa kisovieti mwaka 1991 na kuundwa kwa mataifa mapya, watu wengi ikiwemo kutoka taifa la Kyrgyzstan walikwama kwenye mipaka mipya iliyokuwa imeanzishwa wakiwa na hati za kusafiria za kisovieti ambazo hazikuwa tena halali kudhihirisha walipozaliwa.

Kwa kuzingatia uzoefu wa familia yake katika kupata uraia na utaifa baada ya kuwasili Uzbekistan kufuatia kuvunjika kwa Umoja wa kisovieti, Ashurov aliunde FVLWB mwaka 2003 kupatia msaada wa kisheria wakimbizi waliokuwa hatarini na waliokuwa hawana utaifa wala nyaraka.

Kwenye maeneo ya kusini mwa Krygyzstan.

“Aliunda vikundi vinavyotembea kutoka eneo moja hadi jingine vikitoa msaada wa sheria kwenye maeneo ya ndani na kusaka watu waliokuwa hatarini,” imesema taarifa ya UNHCR.

Vikundi hivyo vilisafiri kwenye milima na mabonde wakiwa kwa magari au farasi na kazi yao kwa ushirikiano na serikali ya Kyrgyzstan imesaidia taifa hilo kutangaza mwezi Julai mwaka huu kuwa halina tena watu wasio na utaifa.