Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu wa UN amelaani vikali shambulio dhidi ya sherehe za kumbukumbu katika mji wa Kerman

Mji wa Kerman ulioko kusini-mashariki mwa Iran
© Unsplash/Mahdi Karbakhsh Ravari
Mji wa Kerman ulioko kusini-mashariki mwa Iran

Mtaalamu wa UN amelaani vikali shambulio dhidi ya sherehe za kumbukumbu katika mji wa Kerman

Haki za binadamu

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran Javaid Rehman amelaani vikali shambulio dhidi ya sherehe za kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa kiongozi nchini Iran Qassem Soleimani katika mji wa Kerman. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu OHCHR jijini Geneva Uswisi Bwana Rehman amesema wale wote waliohusika na mashambulizi mabaya yaliyotokea siku ya jumatano nchini Iran na kuua zaidi ya watu 100 lazima wawajibishwe. 

“Ninalaani mashambulizi haya kwa nguvu zote. Mauaji ni mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya maadili ya kimataifa ya haki za binadamu. Kwa hivyo ni muhimu kuheshimiwa kwa haki za binadamu na utawala wa sheria kuwa msingi wa mapambano ya kimataifa dhidi ya mashambulizi hayo,” alisema mtaalamu huyo. 

Pia Bwana Rehman ametuma salamu za rambirambi na pole kwa familia za wahanga na wananchi wa Iran.

Kuhusu shambulio 

Kwa mujibu wa duru mbalimbali za habari, kulikuwa na milipuko miwili wakati maelfu ya watu wakitembea kuelekea kwenye makaburi ya Kerman, ambayo ni mahali alipozikwa Qassim Suleimani, ambaye aliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani katika mji mkuu wa Iraq wa Baghdad miaka minne iliyopita.

Shambulio hilo limeripotiwa kuuwa zaidi ya watu 100 walioshiriki katika kumbukumbu ya kifo cha jenerali mkuu huyo wa zamani wa kijeshi.

Zaidi ya watu 183 waliokuwa katika eneo la tukio pia wamejeruhiwa kwa mujibu wa maafisa wa Iran. 

Hata hivyo, kutokana na ukubwa wa milipuko hiyo, kuna uwezekano kwamba idadi ya vifo ikaongezeka.