Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde Iran msimnyonge Javid Dehghan: OHCHR

Mtaalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mastaifa ametoa wito wa kuachiliwa watu wanaoshikiliwa kwa kuandamana Shiraz, Iran
UNsplash/Ali Barzegarahmadi
Mtaalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mastaifa ametoa wito wa kuachiliwa watu wanaoshikiliwa kwa kuandamana Shiraz, Iran

Chonde chonde Iran msimnyonge Javid Dehghan: OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR leo imeitaka serikali ya Iran kusitisha mara moja hatua ya kutaka kumnyonga raia wa nchi hiyo anayedaiwa kuteswa hadi kukiri  kwamba ni mwanachama wa kundi la jihadi.

Wito huo uliotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu umekuja siku moja tu kabla ya Javid Dehghab kunyongwa, kufuatia mfululizo wa kutekeleza hukumu ya kifo kwa takribani watu 28 mwezi Desemba waliohukumiwa kunyongwa , wakiwemo watu kutoka makundi ya walio wachache kama wa kutoka kabila la Baluchi ambalo ndilo kabila la Dehghan.

OHCHR imelaani vikali kitendo hicho cha serikali cha kutekeleza hukumu za vifo.

Ofisi hiyo imeitaka serikali ya Iran kutathimini upya kesi ya Bwana. Dehghan kwa kuzingatia sheria za haki za binadamu huku ikiainisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika kesi yake.

Imeongeza kuwa Dehghan alikamatwa mwezi Mei mwaka 2017 na kuhukumiwa kifo kwa kubeba silaha kwa lengo la kukatili maisha au kuharibu mali na kuzusha hofu kubwa.”

Mateso na kutengwa

Kwa mujibu wa OHCHR baada ya kuwekwa rumbane kwenye chumba cha kutengwa peke yake kwa miezi 15 na kuteswa, Bwana Dehghan alikiri  na baadaye kukana kuwa mwanachama wa kundi la jihad na kwamba aliwapiga risasi na kuwaua maafisa wawili wa kikosi cha ulinzi

Licha ya maombi ya kukata rufaa, kesi yake haikufanyiwa tathimini imesema ofisi ya haki za binadamu. 

Mwezi Desemba 2020 wakili wa Dehghan aliwasilisha ombi la kufanyiwa tathimini kwa misingi ya ukiukwaji wakati wa mchakato uliopelekea mteja wake kukutwa na hatia na kuhukumiwa.

Rufaa hiyo ilikataliwa na mahakama kuu ya Iran na wakili huyo amearifiwa siku nne zilizopita.

Wakati akiandaa maombi mapya ya kusikilizwa kwa kwa kesi hiyo wakili alijulishwa kwamba mteja wake ambapengiwa kunyongwa tarehe 30 Januari na ameshaijulisha familia yake kumtembelea kwa mara ya mwisho.