Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kukatwa vidole Iran, wafungwa hatihati kukatwa mkono mzima

Taswira ya mji mkuu wa Iran, Tehran
© Unsplash/Hosein Charbaghi
Taswira ya mji mkuu wa Iran, Tehran

Baada ya kukatwa vidole Iran, wafungwa hatihati kukatwa mkono mzima

Haki za binadamu

Wakati Iran ikiwa katika harakati za kuwakata vidole vyote vya mkononi wafungwa 8 baada ya kupatikana na hatia ya wizi, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR imeelezea wasiwasi wake huku ikitaka serikali ya Iran ifutilie mbali mpango huo.

Msemaji wa OHCHR mjini Geneva, Uswisi, Ravina Shamdasani amesema kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini humo kuwa, “wafungwa hao 8 tayari wameshakatwa vidole vinne vya mkono wa kulia na hivyo wamesalia na dole gumba na kiganja tu kwenye mkono huo wa kulia.”

Ameongeza kuwa wafungwa saba kati yao 8 wanashikiliwa kwenye gereza kuu la Tehran, mji mkuu wa Iran, ilhali mmoja wao hadi sasa hajulikani aliko baada ya kuhamishwa kutoka gereza hilo tarehe 12 mwezi huu.

Kuna mtambo wa kukata vidole

Kwa mujibu wa Bi, Shamdasani, wafungwa wote 8 wanaweza kuhamishiwa kwenye gereza la Evin lililoko mjini Tehran ambako taarifa zinadokeza kuwa, “mtambo wa kukata vidole uliwekwa hivi karibuni na ulitumika tarehe 31 mwezi uliopita wa Mei kukata vidole vya mfungwa mmoja.

“Jaribio la kwanza la kuhamisha wafungwa hao lilifanyika tarehe 11 mwezi huu wa Juni lakini lilisitishwa kutokana na upinzani kutoka kwa wafungwa wenzao.

Mashirika ya kiraia nchini Iran yameripoti kuwa takribani watu 237 nchini humo, wengi wao kutoka jamii za kimaskini wamehukumiwa adhabu ya kukatwa vidole kati ya tarehe 1 Januari hadi tarehe 24 mwezi Septemba mwaka 2020 na kwamba hukumu hizo zimetekelezwa kwa watu 129. 

Iran ni mwanachama wa makubaliano ya kimataifa ya haki za kiraia na kisiasa ambayo Ibara ya 7 inazuia mateso au ukatili wowote au adhabu ya kushusha utu wa kibinadamu.