Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano: SOFEPADI ilivyomsaidia manusura wa ukatili wa kingono Ituri, nchini DRC

Julienne Lusenge, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Kongo ambaye ni rais wa kundi la Sofepadi na mkurugenzi wa Mfuko wa Wanawake wa Kongo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake katika migogoro. (Maktaba - 25 Febr…
UN Photo/ Jean Marc Ferré
Julienne Lusenge, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Kongo ambaye ni rais wa kundi la Sofepadi na mkurugenzi wa Mfuko wa Wanawake wa Kongo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake katika migogoro. (Maktaba - 25 Februari 2019)

Mahojiano: SOFEPADI ilivyomsaidia manusura wa ukatili wa kingono Ituri, nchini DRC

Haki za binadamu

Ukatili wa kingono vitani ni jambo linalokumba wanawake, na wasichana Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Wanapobakwa na kupewa  ujauzito wengi wao hukosa pa kukimbilia kusaka msaada wa kiafya na kisaikolojia. Julienne Lusenge, mshindi wa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu kwa mwaka 2023 kwa kutambua hilo mwaka 2000 aliunda SOFEPADI, shirika la kiraia la kusaidia wanawake na watoto waliokumbwa na ukatili wa kingono na ubakaji. 

Takribani miaka 23 sasa mafanikio yanaonekana. George Musubao, Mwandishi wa Habari wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa nchini DRD amezungumza na mmoja wa wanufaika akiwa ofisi ya SOFEPADI hapa Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Miongoni mwao ni mfanyabiashara ndogo ndogo nyumbani kwangu kama vito na mkaa ambaye George alimuuliza kuliko amefika SOFEPADI.

Mnufaika: Nimefika hapa SOFEPADI kutokana na magumu yaliyonifika. Nilitekwa nyara na waasi wa ADF/NALU. Waasi hawa wanipeleka msituni mimi na wenzangu. Tulikuwa wengi sana. Kwenye familia yetu tulikuwa wanne ambapo wavulana wawili na msichana mmoja waliuawa mbele yangu. Nilibakia peke yangu na niliishi msituni.  Nilipitia machungu mengi sana kwenye kipindi chote cha miaka minne katikati ya waasi hao wanaume. Hakukuweko na njia ya kutoroka. Hatukuwa na kitu na maisha yalikuwa ya kifukara. Kuna wakati wiki ilipita bila hata kula kitu chochote.

George: Siku moja isiyo na jina, mambo yakabadilika..

Mnufaika: Ilikuwa ni siku nzuri ambayo Mungu alituonea huruma kwani baada ya mfululizo wa mashambulizi, nilijikuta niko peke yangu msituni, kwa sababu tulikuwa tumesambaa huku na kule. Nikadhani nimetoroka. Lakini wakati bado niko msituni, nililazimishwa kuishi na mwanaume wa kundi la waasi la ADF awe kama mume wangu. Alinipatia ujauzito. Lakini baadaye nilitoroka nikiwa na ujauzito huo.

George: Baada ya kutoroka msituni ukiwa na ujauzito, ulifikaje hapa SOFEPADI ?

Mnufaika: Katika mazingira hayo magumu, baada ya kurejea kwenye familia yangu, tulikuwa na rafiki ambaye alifika kutufariji. Na tulipomsimulia kisa chote kilichotupata, alitueleza kuhusu shirika hili SOFEPADI ambalo husaidia watu waliokumbwa na masahibu kama yangu. Na ndio sababu familia yangu ilinileta hapa.

George: SOFEPADI husaidia manusura wa ukatili wa kingono ikwemo wale waliobakwa kwenye mazingira ya vita, na bila shaka walikupatia msaada..

Mnufaika: Mara tulipowasili tu hapa walitupokea kwa mikono miwili. Tulielezea kila kitu kilichotufika na walijitahidi kwa kadri ya uwezo wao. Jambo la kwanza walinifanyia uchunguzi baada ya kuona hali mbaya niliyokuwa nayo. Nilikuwa na utapiamlo na wakati huo huo mjamzito. SOFEPADI walinichunguza afya yangu bila gharama yoyote. Walinielekeza pia kwa mtaalamu wa saikolojia ambaye alinipokea vizuri na tulizungumza sana. Taratibu ujasiri ukaanza kunirejea. SOFEPADI wamenisaidia mno. Pindi nilipokuwa na changamoto za kujifungua, walinifanyia upasuaji na kusimamia matibabu yangu ambayo waligharamia, na vivyo hivyo mahitaji ya mtoto. Wiki nzima nilisalia kwenye wodi ya wazazi kwa ajili ya uangalizi. 

George: Huduma hii ya uangalizi haikuishia hapa kwani Neema anasema.

Mnufaika: Na hata niliporejea nyumbani, waliniita ili nije nichukue kiasi cha fedha kwa ajili ya kujikimu na kununua sabuni ya mtoto. Walinipatia pia kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kuanzisha shughuli za kiuchumi. Na ni kwa fedha hizo nikaanzisha biashara, nashukuru sana SOFEPADI.

George: Nikamuuliza Neema, ana ujumbe gani kwa Umoja wa Mataifa?

Mnufaika: Kwa Umoja wa Mataifa kwanza kabisa nawashukuru sana kwa jinsi wanavyosaidia mashirika mbalimbali. Miongoni mwao SOFEPADI. Ningependekeza kwa Umoja wa Mataifa tunataka amani DRC. Tunaipenda nchi yetu lakini tunataka amani. Hakuna amani. Sisi tunatoka jimbo la Ituri hapa ambako hakuna amani. Tunataka hiyo amani jimboni kwetu. Tunataka Umoja wa Mataifa na serikali ya DRC warejeshe amani. Kunapokuweko na shida kama ambazo nimepitia, tunataka Umoja wa Mataifa uweze kutuunga mkono na kutusaidia kama ambavyo imekuwa ikifanya kupitia SOFEPADI.